Nov 28, 2020 11:44 UTC
  • Umoja wa Ulaya walaani mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran

Umoja wa Ulaya umelaani mauaji ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya mwanasayansi wa nyuklia na masuala ya kiulinzi wa Iran na kusema kuwa huo ni uhalifu unaokinzana na msingi wa kuheshimiwa haki za binadamu.

Umoja wa Ulaya leo Jumamosi umetoa taarifa maalumu ya kulaani kuuliwa shahidi mwanasayansi huyo wa nyuklia wa Iran ambapo mbali na kutoa mkono wa pole kwa familia za mashahidi wa shambulio hilo la kigaidi umewaombea majeruhi afueni ya haraka.

Taarifa hiyo ya Umoja wa Ulaya imesema, tarehe 27 Novemba 2020 na katika eneo la Absard, afisa mmoja wa serikali ya Iran na raia kadhaa wameuawa katika majimui ya mashambulio ya kuua. Huo ni uhalifu na unakinzana na msingi wa kuheshimu haki za binadamu ambao unaungwa mkono na Umoja wa Ulaya.

Ofisi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji

 

Mwishoni mwa taarifa yake, Umoja wa Ulaya umetaka pande zote kuwa wavumilifu na kusisitiza kuwa, katika wakati huu usio mtulivu, kuna wajibu kila upande kuwa na uvumilivu kuliko wakati mwingine wowote ili kuiepusha dunia na machafuko yoyote ambayo kimsingi si kwa faida ya mtu yeyote yule.

Kabla ya hapo pia, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa Bi Agnès Callamard ameyataja mauaji ya kigaidi ya mwanasayansi  wa masuala ya nyuklia na ulinzi wa Iran Shahidi Mohsen Fakhrizadeh kuwa "mauaji ya nje ya mipaka yaliyofanywa kwa lengo maalumu" na akasisitiza kuwa, kumkosesha mtu haki ya kuishi katika kipindi cha amani ni ukiukaji wa Hati ya Umoja wa Mataifa.

Wakati huohuo mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameliandikia barua Baraza la Usalama la umoja huo akisisitiza kwamba utawala wa Kizayuni ndio unaobeba dhima ya mauaji ya mwanasayansi wa nyuklia wa Iran shahidi Mohsen Fakhrizadeh. 

Tags