Dec 02, 2020 07:11 UTC
  • Kikao kijacho UN ni cha kadhia ya nyuklia ya Iran, A/Kusini ndiye mwenyekiti

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kuitisha kikao maalumu cha kujadili makubaliano ya nyuklia ya Iran mwishoni mwa mwezi huu wa Disemba.

Shirika la habari la TASS limeripoti habari hiyo na kumnukuu Jerry Matthews Matjila, mwakilishi wa kudumu wa Afrika Kusini katika Umoja wa Mataifa ambaye nchi yake ndiye mwenyekiti wa hivi sasa Baraza la Usalama la umoja huo akisema kwamba, kikao cha kujadili mapatano ya nyuklia ya Iran kitafanyika tarehe 22 mwezi huu wa Disemba katika baraza hilo.

Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei 2018, rais wa Marekani, Donald Trump aliitoa kijeuri nchi hiyo katika mapatano hayo yanayojulikana kwa jina maarufu la JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kufanikisha kufikiwa kwake. Baada ya hapo Trump aliirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo. 

Mradi wa nyuklia wa Iran ni wa amani kikamilifu

 

Hata hivyo hatua hiyo ya kibeberu na iliyoonesha chuki za kupindukia za Trump dhidi ya taifa la Kiislamu la Iran imelaaniwa vikali ndani ya Marekani kwenyewe na kimataifa.

Sasa hivi na baada kubwagwa Donald Trump katika uchaguzi wa Novemba 3, 2020 huko Marekani na Joe Biden kuchaguliwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo, kumeanza mjadala mpya kuhusu uwezekano wa kurejea Marekani katika mapatano ya JCPOA na kuendelezwa yale yaliyokubaliwa katika makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa mwaka 2015.

Tags