Dec 03, 2020 02:37 UTC
  • Serikali ya Ufaransa yafutilia mbali muswada wa marufuku ya kupigwa picha polisi

Serikali ya Ufaransa imefutilia mbali muswada iliokuwa umeuwasilisha bungeni kwa ajili ya kupiga marufuku upigwaji picha maafisa wa polisi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao, na hilo limetokana na ukosolewaji mkali uliofanywa dhidi ya utendaji wa jeshi la polisi.

Christophe Castaner, mkuu wa chama tawala cha Ufaransa amesema kuwa muswada huo utaandaliwa na kuwasilishwa upya bungeni.

Muswada uliofutiliwa mbali ulikuwa na vipengee 32 vinavyoongeza mamlaka ya polisi na maafisa usalama wanaolinda usalama katika sekta binafsi ambapo pia ulikuwa unalenga kuwaandalia wanasheria ambao wangewatetea mbele ya vyombo vya mahakama katika operesheni zao za kulinda usalama na utumia wa ndege zisizokuwa na rubani.

Pamoja na hayo ni kipengee cha 24 cha muswada huo ndicho kimezua utata. Kipengee hicho kilikuwa kinapiga marufuku polisi au wanajeshi kupigwa picha wakati wanapotekeleza operesheni za kulinda amani na kukabiliana na wanaozua ghasia, jambo ambalo lingefichua nyuso zao na hivyo kuhatarisha maisha yao. Kipengee hicho kilikuwa kinatoa adhabu ya kufungwa jela mwaka mmoja au kutozwa faini ya Euro 45,000 kila ambaye angekiuka sheria hiyo.

Gabriel Attal, Msemaji wa Serikali ya Ufaransa amesema kuwa muswada huo ulikuwa inalenga kuwalinda polisi ambao wamekuwa wakishambuliwa na sio kupiga marufuku upigaji picha operesheni za polisi wakati wa maandamano, lakini pamoja na hayo umepingwa vikali na wananchi wa Ufaransa na vilevile taasisi za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo chama cha waandidhi wa Ufaransa kimepinga muswada huo kikisema kuwa ni mfano halisi wa kubana uhuru wa kijieleza na upashaji habari.

Maandamano Ufaransa

Taasisi zinazopinga utumiaji mabavu na nguvu ya ziada kutoka kwa polisi pia zimesema kuwa kipengee hicho kinachopiga marufuku polisi kupigwa picha wanapotekeleza operesheni za kukabiliana na waandamanaji ni hatua ya kujaribu kubana matumizi ya picha na video zinazochukuliwa na waandishi wakati wa maandamano, jambo ambalo linaweza kusadia katika utoaji ushahidi wa kuthibitisha mabuvu yanayotumiwa na polisi katika kukabiliana na waandamanaji.

George Pau-Langevin, mbunge wa chama cha Kisoshalisti katika bunge la Ufaransa amesema kuhusu suala hilo kwamba: Matokeo ya moja kwa moja ya muswada huo ni kubanwa pakubwa uhuru wa upashaji habari na vyombo vya habari.

Katika uwanja huo, maelfu ya Wafaransa waliandamana katika zaidi ya miji 70 ya nchi hiyo mwanzoni mwa wiki iliyopita, baada ya kusambazwa katika mitandao ya kijamii picha na video zilizoonyesha jinsi raia mmoja mwenye asili ya Kiafrika alivyokuwa akipigwa kinyama na kushughulikiwa na polisi wasio na huruma, maandamano ambayo yaligeuka na kuwa ya ghasia.

Wapinzani wanasema muswada huo unabana na kuwanyima uhuru wa kufanya kazi zao za upashaji habari na wakati huo huo kuwakinga polisi wanaotumia mabavu dhidi ya waanadamani na kukiuka haki zao za kibinadamu, dhidi ya kuwajibishwa mbele ya sheria.

Christophe Deloire, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Maripoti Wasio na Mipaka ametumia kinaya kuhusu utumiaji mabavu wa polisi ya Ufaransa kwa kusema: Nchi ya haki za binadamu badala ya kutumia vitisho inapasa kuwalinda waaandishi wake na kusisitiza kuwa mabavu hayo ya polisi hayakubaliki kabisa.

Unyama wa polisi ya Ufaransa dhidi ya waandamanaji

Katika miaka ya karibuni, vitendo vya polisi ya Ufaransa kutumia mabavu na nguvu ya ziada vimekuwa vikiongezeka sana ambapo ripoti chungu nzima zimetolewa kuhusu mabavu yanayotumiwa na polisi dhidi ya watu weusi, wahajiri na wanaharakati wa masuala ya kijamii. Hii ni katika hali ambayo Ufaransa imekuwa ikidai kuwa ni mtetezi mkuu wa haki za binadamu na uhuru wa mtu binafsi na wa kijamii. Katika uwanja huo tunaweza kuashiria msimamo wa karibuni wa Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo wa kutetea vikatuni vilivyodhalilisha na kumvunjia heshima Mtume Mtukufu (saw) kwa kisingizio cha eti kutetea uhuru wa kujieleza.

Hivi sasa kuongeza malalamiko ya ndani na ukosoaji wa nje ya Ufaransa umeilazimisha serikali ya Paris kurejea nyuma na kufutilia mbali muswada wake uliokuwa unabana wazi wazi uhuru huo aliodai kuutetea Macron. Ni wazi kuwa hata kama viongozi wa Ufaransa wanadai kutetea uhuru na demokrasia nchini humo lakini kufichuliwa hivi karibuni vitendo vya utumiaji mabavu vya polisi kumebatilisha wazi nara na madai hayo yasiyokuwa na ukweli wowowe.

 

Tags