Dec 03, 2020 11:07 UTC
  • Umoja wa Mataifa wapasisha matumizi ya bangi kwa ajili ya matibabu

Tume ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na kudhibiti mihadarati imepiga kura na kupasisha matumizi ya bangi kwa ajili ya matibabu.

Upigaji kura huo umefanyika baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kupendekeza kuongolewa bangi katika orodha ya kundi la dawa hatari zaidi za kulevya. Hatua ya Umoja wa Mataifa ya ya kupasisha pendekezo hilo la WHO, itachochea uzalishaji wa bangi kwa matumizi ya kimatibabu.

Kati ya nchi 53 wanachama, 27 zilipiga kura ya kuunga mkono mapendekezo hayo WHO na nchi 25 zilipinga. Ukraine ilikuwa nchi pekee ambayo haikupiga kura.  Miongoni mwa mataifa yaliyopiga kura ya kuunga mkono mapendekezo hayo, ni Marekani na nchi za Ulaya huku China, Misri, Nigeria, Pakistan na Russia zikiwa miongoni mwa nchi zilizopinga kuhalalisha mmea huo.

Vita dhidi ya mmea wa bangi nchini Tanzania

 

Hatua hiyo inatarajiwa kufungua milango kwa mmea wa bangi kutambulika rasmi kuwa na manufaa kama ya dawa na tiba na pia itakuwa rahisi kwa nchi mbalimbali kuufanyia utafiti mmea huo.

Mwezi Oktoba mwaka huu, serikali ya Rwanda ilitangaza kuwa, imehalalisha kisheria ukulima na mauzo ya nje ya nchi ya mmea wa bangi kwa ajili ya matumizi ya tiba ili kupata fedha.

Akizungumza na televisheni ya taifa ya nchi hiyo, Waziri wa Afya wa Rwanda Dk. Daniel Ngamije alisema mimea ya matitabu iliyoruhusiwa nchini humo inajumuisha pia mmea wa bangi.

Kabla ya Rwanda, nchi kama Malawi, Lesotho, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe zilikuwa tayari zimepitisha kisheria za kuruhusu mauzo ya bangi au matumizi ya mmea huo ambao una madawa ya kulevya.