Dec 04, 2020 00:15 UTC
  • Madai ya kukaririwa ya Ulaya kuunga mkono JCPOA; nara tupu zisizofungamana na vitendo

Licha ya kuwa baada ya kujitoa marekani katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia maarufu kama JCPOA, nchi za Ulaya zimekuwa na utendaji hasi na dhaifu katika kulinda na kutekeleza ahadi zao kuhusu mapatano hayo, lakini zingali zinadai kwamba zinaendelea kuyalinda.

Joseph Borell, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya siku ya Jumanne alisisitiza kwa mara nyingine tena umuhimu wa kulindwa mapatano hayo ya nyuklia na kuandika kupitia ujumbe wa Twitter kwamba: "Katika mazungumzo yangu na Muhammad Jawad Zarif (Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran), nimesisitiza umuhimu wa kulinda mapatano ya JCPOA. Nikiwa mratibu wa kutekelezwa mapatano hayo, nitadumisha juhudi zangu za kuhakikisha kwamba pande zote zinatekeleza wajibu wao kikamilifu."

Madai hayo yametolewa na Borell katika hali ambayo baada ya Marekani kujitoa katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei 2018, Umoja wa Ulaya si tu kwamba haujachukua hatua yoyote ya kupunguza taathira hasi za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bali nchi na mashirika ya umoja huo yamekuwa yakitekeleza vikwazo hivyo vya kidhulma kwa kuogopa kuadhibiwa na serikali ya Washington.

Joseph Borell

Inaonekana kuwa Borell amewasiliana na waziri wa mambo ya nje wa Iran na kumsisitizia udharura wa kulindwa mapatano ya JCPOA kutokana na uamuzi wa hivi karibuni wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge), wa kupitisha muswada wa kuondolewa vikwazo dhidi ya Tehran. Jumanne bunge hilo lilipitisha kwa wingi wa kura muswada ambao unaitaka serikali ya Iran ianze kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 20 na wakati huo huo kusimamisha utekelezaji wa protokali ziada ya mkataba wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia NPT, iwapo pande za mapatano ya JCPOA zitaendelea kupuuza uwajibikaji na ahadi zao kwa Iran. Muswada huo umepitishwa kufuatia hatua za kiuadui za Marekani dhidi ya Iran kwa ushirikiano wa nchi za Ulaya. Muswada huo umeupa Umoja wa Ulaya muda wa mwezi mmoja uwe umeanza kutekeleza ahadi zake kwa Iran na kuiondolea vikwazo vyote.

Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuitoa nchi hiyo katika mkataba wa JCPOA, Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya hazijachukua hatua yoyote ya kutekeleza ahadi zao wala kujaribu kupunguza taathira hasi za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran bali zimeendelea kusalia katika mapatano hayo kidhahiri tu na hata mara nyingine kuhisi kwamba zinaidai Iran. Zimekuwa zikidai mara kwa mara kwamba kwa kutilia maanani umuhimu wa mkataba wa JCPOA katika kudhamini amani na usalama wa kieneo na kimataifa zimeazimia kuyalinda matano hayo ya nyuklia na kutoa ahadi za uongo kwamba zitafanya juhudi zao zote ili kuyalinda.

Mfumo wa kibiashara na kifedha wa Instex

Kwa mujibu wa Jin Liang Chiang, mtafiti wa ngazi za juu wa Uchina, mapatano ya JCPOA ni mfano muhimu wa mafanikio ya Umoja wa Ulaya, lakini kwa kujitoa katika mapatano hayo, Trump ameharibu juhudi na matunda hayo yote muhimu ya Umoja wa Ulaya na kutoa pigo kubwa kwa nchi wanachama wa Umoja huo, kama washirika muhimu wa kutatuliwa kwa amani hitilafu na migogoro ya kimataifa.

Tathmini kuhusu misimamo ya nchi za Ulaya baada ya kujitoa Marekani JCPOA inabainisha wazi kuwa nchi hizo zimeshindwa kabisa kutekeleza ahadi zilizotoa kwa Iran. Kutokana na mashinikizo ya Marekani na pia kwa kutokuwa na azma thabiti, nchi hizo zimekataa kutekeleza ahadi zao na hasa mfumo wa mabadilishano ya kibiashara na kifedha kati yazo na Iran, mashuhuri kama Instex. Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa katika hatua ya kwanza utekelezaji wa mapatano ya JCPOA umekwama kutokana na siasa za uhasama na mashinikizo ya hali ya juu kabisa ya Marekani dhidi ya Iran na katika hatua ya pili ni kutokana na nchi za Ulaya kutotekeleza ahadi zao kwa Iran kwa msingi wa mapatano hayo.

Tags