Dec 04, 2020 06:55 UTC
  • Umoja wa Mataifa waitambua rasmi serikali ya Maduro

Licha ya uchochezi na mashinikizo yanayotolewa na Marekani kwa ajili ya kupoteza itibari ya serikali ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela, Umoja wa Mataifa umetangaza wazi kuwa unaitambua rasmi serikali hiyo kuwa mwakilishi pekee halali na wa kisheria wa taifa la Venezuela.

Hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa imechukuliwa katika hali ambayo serikali ya Venezuela na hasa katika miaka minne ya karibuni imekuwa chini ya mashikizo makubwa ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa lengo la kuipindua na kuiondoa madarakani kinyume cha sheria. Trump ametumia mbinu tofauti zikiwemo za vikwazo vya kiuchumi, jaribio la mapinduzi, kuharibu miundomsingi mikuu na hasa ya usambazaji umeme, kuunga mkono wapinzani na vitisho vya kijeshi kwa ajili ya kumshinikiza Maduro aondoke madarakani. Mashinikizo hayo yalifikia kilele pale Marekani ilipomtambua kinyume cha sheria, Juan Guido, kiongozi wa upinzani wa Venezuela kuwa rais wa nchi hiyo na kuwataka washirika wake pia waige mfano huo.

Waungaji mkono wa Maduro

Katika uwanja huo, Marekani ilimpa Juan Guido kila aina ya msaada wa kisiasa na kifedha kwa kadiri kwamba ilimualika nchini Marekani kama rais wa Venezuela na kumpa mapokezi yote rasmi anayostahili rais wa nchi. Licha ya uungaji mkono huo wote wa hali na mali lakini Guido hakuweza kudhamini maslahi ya kisiasa ya Washington kama alivyotarajiwa, jambo lililompelekea Trump kukata tamaa na kusema hadharani kwamba hakuwa tena na imani na kiongozi huyo wa upinzani wa Venezuela.

Ama kwa kweli wananchi wa Venezuela hawakuweza kumkubali Juan Guido kama kiongozi wao jambo ambalo liliibua hitilafu katika mrengo wa upinzani na hivyo kumpotezea imani na uungaji mkono katika mrengo huo.

Juan Carlos Hidalgo, mtaalamu wa masuala ya siasa ya Latin Amerika anasema kuhusu suala hilo kwamba: Senerio ya kumtafuta mbadala wa Rais Nicolas Maduro wa Venezuela si ya kweli.

Hii ni katika hali ambayo hata katika mazingira ya hivi sasa ya kuenea virusi vya corona ulimwenguni, lakini vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela bado vinaendelea. Watawala wa Marekani bado wanatumai kwamba janga la virusi hivyo litasaidia kuvuruga zaidi hali ya mgogoro wa uchumi wa Venezuela na hivyo kuharakisha kusambaratika nchi hiyo ndani kwa ndani. Kinyume na matarajio ya Marekani, wapinzani wengi wa Maduro wanakosoa vikali vikwazo hivyo wakisema kuwa vinawatesa tu wananchi wa kawaida wa Venezuela bila ya kuleta madadiliko yoyote ya kisiasa ndani ya nchi.

Juan Guido (kulia) anayetumiwa na Trump kuvuruga amani ya Venezuela

Jeffrey Sachs, mwanauchumi mashuhuri wa Marekani ambaye pia ni mwanastratijia wa maenedeleo endelevu anaashiria athari hasi za vikwazo vya kiuchumi vya Marekani katika kukabiliana na janga la corona na hasa kwa nchi kama vile Venezuela na kusisitiza udharura wa kukomeshwa vikwazo hivyo katika mazingira ya sasa. Anasema, iwapo vikwazo hivyo vitaendelea ni wazi kuwa taathira zake hasi zitawakumba wote waliomo na wasiokuwamo.

Hivi sasa hatua ya Umoja wa Mataifa ya kumtambua rasmi Nicolas Mduro kama Rais halali wa Venezuela kwa mara nyingine tena imevunja njama na chokochoko za kikoloni za serikali ya Trump dhidi ya Venezuela na wakati huo huo ni ushindi mkubwa kwa serikali ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Ni wazi kuwa siasa za uhasama za serikali ya Marekani dhidi ya Venezuela zimepata pigo kubwa kiasi kwamba hata jamii ya kimataifa imekataa kuzikubali.