Dec 27, 2020 02:32 UTC
  • Kupitishwa maazimio 17 ya Baraza la Kuu la UN dhidi ya Israel katika mwaka 2020

Utawala wa Kizayuni ni utawala pekee uliolaaniwa na Umoja wa Mataifa mara tatu zaidi ya nchi nyingine zote duniani katika mwaka huu wa 2020. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha jumla ya maazimio 17 dhidi ya Israel katika mwaka huu wa 2020.

Gazeti la Times of Israel limeinukuu taasisi moja inayoukingia kifua utawala wa Kizayuni na kueleza kuwa: Umoja wa Mataifa katika mwaka huu wa 2020 kwa pamoja  uliwasilisha maazimio na kuzilaani mara 23 nchi mbalimbali duniani ambapo miongoni mwake  maazimio 17 yaliuhusu utawala wa Kizayuni pekee na yaliyosalia yalizihusu nchi nyingine tano duniani. 

 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limewasilisha maazimio 17 dhidi ya Israel kwa sababu ya jinai za hujuma zinazofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya nchi tatu za Palestina, Syria na Lebanon. Jinai na uvamizi huo vinahusiana na masuala ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, kukaliwa kwa mabavu kijiografia, kupuuzwa haki za kuainisha mustakbali, suala la wakimbizi, kubadilishwa mipaka na masuala ya kiuchumi na kifedha. 

Wakimbizi wa Kipalestina katika kambi nchini Syria  

Maazimio yaliyopasishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni ya hiari katika utekelezaji wake lakini yana jumbe mbili muhimu ndani yake. Wa kwanza ni kudhihirisha wazi utambulisho halisi ya utawala wa Kizayuni utendao jinai; na ujumbe wa pili ni kuwa: maazimio hayo yanaonyesha kwamba jamii ya kimataifa inachukua hatua za kukabiliana na utawala huo licha ya propaganda kubwa zinaoendeshwa kuhusiana na uhusiano mkubwa uliopo kati ya utawala wa Kizayuni na nchi mbalimbali. Kuhusiana na suala hilo Riyadh al Maliki Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina anasema: kupasishwa maazimio yote hayo kunaonyesha namna jamii ya kimataifa ilivyo na msimamo thabiti mkabala na haki za tafa la Palestina, wakimbizi na pia jinsi inavyokabiliana na vitendo na jinai za Israel dhidi ya raia wa Palestina.  

Riyadh al Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina  

Suala jingine ni kuwa, maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa dhidi ya Israel yamewasilishwa chini ya kivuli cha hatua za uungaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu. Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 28 Januari mwaka huu ilizindua mpango ilioupa jina la Muamala wa Karne. Mpango huo pamoja na kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni umeunga mkono pia vitendo vya ukaliaji ardhi kwa mabavu vya utawala huo katika kuitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa Israel, umeunga mkono kutambuliwa rasmi mamlaka ya utawala wa Israel katika miinuko ya Golan ya Syria na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.  

Mbali na hayo, Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco ni nchi nne ambazo katika miezi mitatu ya mwisho wa mwaka huu wa 2020 zimeanzisha uhusiano rasmi na Israel. Saudi Arabia ambayo inadai kuwa ni kiranja wa Ulimwengu wa Kiarabu pia imeunga mkono mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel. Kuanzishwa mahusiano hayo kunadhihirisha wazi jambo hili kwamba, nchi za Kiarabu ziko bega kwa bega na Israel; na wala hazihisi lolote kuhusu jinai zinazofanywa na utawala huo dhidi ya nchi za Kiarabu khususan Palestina. Kwa msingi huo, jinai za utawala wa Israel dhidi ya Palestina, Syria na Lebanon katika mwaka huu wa 2020 zimeongezeka. 

Miinuko ya Golan huko Syria inayokaliwa kwa mabavu na Israel 

Jambo jingine ni kwamba, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu wa 2020 limepasisha maazimio 17 dhidi ya Israel huku Baraza la Usalama la umoja huo pia likiwa limekaa kimya bila kupasisha hata azimio moja dhidi ya Israel. Tukio hilo pia lina nukta kadhaa muhimu. Ya kwanza: Ni kwa kiwango kidogo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linafanya mambo kwa "utashi wa kisiasa" kulinganisha na Baraza la Usalama la umoja huo. Nukta ya pili ni kuwa: kwa sababu hakuna kura ya veto ndani ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inawezekana kirahisi kupasishwa azimio dhidi ya jinai za Israel, na nukta ya tatu ni kuwa: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limehodhiwa na Marekani; na siasa za Marekani zinaikwamisha taasisi hiyo ya kimataifa kutekeleza majukumu yake makuu yaani kulinda na kudumisha amani na usalama duniani kote.  

 

Tags