Jan 12, 2021 02:32 UTC
  • Ujumbe na malengo ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Falih al-Fayadh

Wizara ya Fedha ya Marekani, siku ya Ijumaa iliweka jina la Falih al-Fayadh, Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya al-Hashd al-Shaabi ya nchini Iraq katika orodha yake ya vikwazo kwa kisingizio cha kukiuka haki za binadamu. Hatua hiyo ya Marekani ina ujumbe muhimu kwa mitazamo kadhaa.

Ujumbe wa kwanza muhimu ni kwamba serikali ya Marekani haikuchukulii kujitawala kwa nchi kuwa moja ya misingi muhimu inayopaswa kuheshimiwa na serikali tofauti za dunia.

Falih al-Fayadh ni mmoja wa viongozi rasmi wa serikali ya Iraq ambaye zamani alikuwa mshauri wa usalama wa taifa wa Iraq na hivi sasa ni mkuu wa harakati ya al-Hashd al-Shaabi. Kwa mujibu wa muswada iliopasishwa na bunge la Iraq 2016, shakhsia na wanasiasa wote wanaohudumu katika harakati ya Hashd al-Shaabi ni miongoni mwa maafisa rasmi wa serikali ya Iraq. Kwa msingi huo harakati ya karibuni ya Marekani ni ukiukaji wa wazi wa kujitawala Iraq, jambo ambalo limekosolewa na kulaaniwa na wanasiasa tofauti wa nchi hiyo.

Kuhusu hilo, Humam Hamuodi, Mkuu wa Majlisi Kuu ya Kiislamu ya Iraq ametoa taarifa akilaani hatua hiyo ya Marekani na kusisitiza kuwa kuwekwa jina la Falih al-Fayadh katika orodha ya vikwazo ya Wizara ya Fedha ya Marekani ni kuzidishwa uchokozi wa nchi hiyo dhidi ya Iraq na kundi la Hashd al-Shaabi na kusema kuwa hilo ni dhihirisho la wazi la kukiukwa utawala wa Iraq.

Falih al-Fayadh

Ujumbe mwingine unaotolewa na hatua hiyo ya Marekani ni kwamba nchi hiyo haiheshimu hata kidogo vyombo vya mahakama vya Iraq. Vyombo hivyo Alkhamisi vilitoa waranti wa kukamatwa Rais Donald Trump wa Marekani kwa kuhusika kwake katika mauaji ya jinai dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC pamoja na Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq, yaliyotekelezwa tarehe 3 Januari mwaka uliopita. Vikwazo dhidi ya al-Fayadh vimetekelezwa siku moja baada ya kutolewa hukumu hiyo dhidi ya Trump jambo ambalo linathibitisha kwamba vimeteklelezwa dhidi ya mwanasiasa huyo wa Iraq kama jibu la Washington kwa hatua hiyo ya vyombo vya mahakama vya Iraq.

Hatua hiyo ya Marekani imetekelezwa kwa sababu kadhaa. Sababu ya kwanza inatokana na ukweli kuwa Marekani imekuwa na chuki ya muda mrefu dhidi ya mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi, hivyo hatua ya  nchi hiyo dhidi ya al-Fayadh imechukuliwa katika muelekeo huo. Serikali ya Marekani imekuwa ikitekeleza siasa za vikwazo na ugaidi dhidi ya mrengo huo kama mbinu muhimu ya kukabiliana na maadui zake na mauaji ya tarehe 3 Januari 2020 dhidi ya Qassem Soleimani na al-Muhandis yalitekelezwa kwa mtazamo huo. Mauaji hayo ya jinai hayapaswi kutathminiwa katika mtazamo wa hujuma dhidi ya Iraq pekee bali yanapaswa kutathminiwa katika mtazamo wa chuki na uadui wa Marekani dhidi mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika upeo mzima wa kieneo.

Sababu nyingine ni kwamba Falih al-Fayadh ni mkuu Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq ambayo ni sehemu rasmi ya jeshi la nchi hiyo na ambayo pia inapinga siasa za Marekani na utawala haramu wa Israel. Harakati hiyo ya Kiislamu inashinikiza askari wa Marekani waondolewe Iraq haraka iwezekanavyo. Falih al-Fayadh ambaye ana misimamo iliyo dhidi ya Marekani na Uzayuni amekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha nguvu ya Hashdu sh-Sha'abi nchini Iraq. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Marekani ikawa inamchukia sana kiongozi huyo na mwishowe kuamua kumuwekea vikwazo.

Qassem Soleimani  (kulia) na al-Muhandis waliouawa kigaidi kwa amri ya Trump

Kwa hatua hiyo, Marekani inafuatilia malengo kadhaa, muhimu zaidi likiwa ni kutaka kuanzisha chuki na mgawanyiko wa kisiasa kati ya viongozi wa Iraq. Kupitia njama hiyo Marekani inataka kuwathibitishia Wairaki kwamba ni Hashdu sh-Sha'abi ndiyo inawasababishia matatizo ya sasa.

Lengo jingine muhimu la Marekani ni kutaka kuzuia kufukuzwa askari wake katika ardhi ya Iraq na kwamba kufuatiliwa jambo hilo kuna gharama kubwa inayopaswa kulipwa.

Pamoja na kuwepo vitisho vyote hivyo lakini hatua hizo za Marekani ambazo ni ikuikaji wa wazi wa kujitawala Iraq, hazitazuia kufukuzwa kwa askari wake kutoka Iraq bali kutaimarisha zaidi azma ya viongozi na makundi ya nchi hiyo ya kufuatilia na kufanikisha lengo la kuondolewa askari hao katika ardhi yao.

Tags