Jan 14, 2021 02:39 UTC
  • Russia yapuuzilia mbali bwabwaja mpya za Marekani dhidi ya Iran

Russia imekosoa vikali madai ya kipropaganda ya Marekani ya kujaribu kulifungamanisha kundi la kigaidi la al-Qaeda na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pasi na kutoa ushahidi wowote.

Katika taarifa jana Jumatano, Zamir Kabulov, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema madai hayo yasiyo na msingi yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo ambaye ameifungamanisha Iran na kundi la kigaidi la al-Qaeda ni ya kipuuzi, yasiyo na mantiki na yasiyokubalika.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amesema Pompeo ametoa porojo hizo bila kutoa taarifa au ushahidi wowote wa kuyapa nguvu madai hayo yake yasiyo na msingi.

Juzi Jumanne, Pompeo alitoa madai yasiyo na msingi kuwa Iran ni kituo cha al-Qaeda na kuongeza kuwa idadi kubwa ya wanachama wa kundi hilo la kigaidi walihamia Iran baada ya matukio ya Septemba 11.

Pompeo alikutana na mkuu wa Mossad ya Israel kabla ya kutoa porojo mpya dhidi ya Iran

Kadhalika  Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif ametoa radiamali yake kuhusu madai hayo yasiyo na msingi ya Pompeo na kusisitiza kuwa: "Magaidi wote wa Septemba 11 walitoka katika nchi anazozipenda Mike Pompeo katika Mashariki ya Kati (Asia Magharibi)."

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Bunge la Congress la Marekani, na ambao ulitayarishwa miezi kadhaa baada ya tukio la Septemba 11, watu 15 kati ya 19 walioteka ndege zilizohusika katika hujuma za mashambulio hayo ya Septemba 11 walikuwa ni raia wa Saudia, wawili walikuwa raia wa Umoja wa Falme za Kiarabu  na wote walikuwa wanafungamana na maafisa wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili ambao waliwapa msaada wa kilojistiki na kifedha.

Tags