Jan 15, 2021 14:19 UTC
  • Muswada wa kumzuia Trump kuingia Congress maisha yake yote

Mbunge wa chama cha Democrat wa jimbo la Georgia amewasilisha bungeni muswada ambao iwapo itapitishwa utamzuia Rais Donald Trump wa Marekani kuweka mguu wake katika Congress ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Russia Today, matukio ya kashfa ya baada ya uchaguzi mkuu wa karibuni nchini Marekani yamewapelekea wabunge wa chama cha Democrat na hasa Nikima Williams wa jimbo la Georgia kuchukua hatua ya kuandaa muswada wa kumtaka Trump apigwe marufuku kushiriki siasa za Marekani.

Kwa mujibu wa muswada huo, polisi ya Congress na walinzi wa mabunge yote mawili ya Congress na Senate watalazimika kumzuia Trump kukaribia majengo ya mabunge hayo mara tu baada ya kuondoka madarakani.

Hii ni katika hali ambayo katiba ya Marekani inazuia kupasishwa muswada unaomlenga mtu maalumu nchini humo. Kwa msingi huo wajuzi wa mambo wanasema kuwa iwapo muswada huo utapitishwa bungeni, litakuwa jukumu la vyombo vya mahakama kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo.

Congress ya Marekani

Kufuatia tukio la kushambuliwa jengo la Congress na wafuasi wa Trump, siku ya Jumatano wabunge walipitisha muswada wa kumsaili Trump kwa kura 229 za ndio na 197 za hapana.

Kura hiyo imemfanya Trump kuwa Rais wa kwanza wa Marekani kuwahi kusailiwa mara mbili katika historia ya nchi hiyo. Kura ya mwisho ya kupitishwa muswada huo itapigwa baadaye katika bunge la Seneti. Bila ya kura hiyo muswada huo hautakuwa na athari yoyote. Iwapo utapitishwa katika bunge hilo, Trump atafutwa kazi na kulazimika kuondoka ofisini.

Katika muswada huo, Trump ametuhumiwa kwa makosa kadhaa makubwa likiwemo la kuwachochea wahuni na wafuasi wake wavamie jengo la Congress ya Marekani.

Tags