Jan 16, 2021 13:14 UTC
  • FBI: Watu zaidi 200 wanashukiwa kutaka kutumia silaha moto kuvuruga sherehe ya kuapishwa Biden

Mkuu wa polisi ya upelelezi ya Marekani FBI amesema, kuna ushahidi wenye kutia wasiwasi juu ya uwezekano wa kufanyika maandamano ya upinzani ya utumiaji wa silaha moto sambamba na hafla ya kuapishwa rais mpya wa nchi hiyo.

Chris Wray ametangaza kuwa, kuna watu zaidi ya 200 ambao FBI imewatambua kuwa wanaweza wakazusha machafuko na kutumia nguvu wakati wa kutawazwa rais mteule Joe Biden katika hafla itakayofanyika wiki ijayo.

Wray amesema, yeye na timu yake wanafuatilia "mawasiliano makubwa yenye kutia wasiwasi yanayofanyika  mitandaoni" yakiwemo ya miito ya kuhamamisha upinzani wa kutumia mtutu bunduki kuelekea Januari 20 ambayo ni siku ya kuapishwa Biden.

Ameonya kuwa, kuna uwezekano wa kutokea maandamano ya fujo na utumiaji nguvu mjini Washington na kusababisha watu wenye silaha kukaribia majengo ya serikali na maafisa wateule.

Chris Wray

Wakati huohuo Anthony Scaramucci, mkurugenzi wa zamani wa mawasiliano katika Ikulu ya White House amekosoa vikali matukio yaliyojiri baada ya uchaguzi wa nchi hiyo na kusema kuwa historia itamkumbuka rais wa Marekani kama mchocheaji wa ugaidi wa ndani.

Scaramucci ameongeza kuwa, Donald Trump ni mtu anayehamaisha uasi na machafuko na ni gaidi wa ndani wa karne 21.

Afisa huyo mwandamizi wa zamani katika serikali ya Trump ametaka rais huyo anayeondoka madarakani ashtakiwe na kuhukumiwa katika Seneti ya nchi hiyo.

Hayo yanajiri huku jeshi la Marekani likitoa taarifa na kutangaza kuwa wizara ya ulinzi Pentagon imetoa kibali cha kutumwa askari zaidi ya 25,000 wa gadi ya taifa kwenda kuvisaidia vikosi vya serikali kuu katika kulinda usalama wakati wa hafla ya kuapishwa rais mpya wa nchi hiyo.

Wakati huohuo uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa unaonyesha kuwa asilimia 90 ya Wamarekani wanapinga uvamizi wa Januari 6 dhidi ya jengo la Bunge na asilimia 70 wamesema, rais wa nchi hiyo Donald Trump anapaswa angalau akubali kubeba dhima ya sehemu ya matukio yaliyojiri katika uvamizi huo.

Wafuasi wa Trump wakivamia jengo la Kongresi ya Marekani

Uchunguzi huo uliofanywa kwa pamoja na televisheni ya ABC News na gazeti la Washington Post  unaonyesha pia kuwa asilimia 56 ya waliotoa maoni yao wanaunga mkono hatua za Kongresi za kutaka kumzuia Trump asiweze kugombea tena urais katika uchaguzi ujao.

Watu wasiopungua sita walifariki katika fujo na machafuko yaliyojiri Jumatano ya tarehe 6 Julai wakati wafuasi wa Trump walipovamia na kulishikilia kwa saa kadhaa jengo la bunge la Marekani.../

Tags