Jan 17, 2021 02:19 UTC
  • Uhasama usio na mwisho wa Marekani dhidi ya Hashdu Shaabi

Marekani imemuwekea vikwazo Abu Fadak al Muhammadawi Naibu Mkuu wa Harakati ya al Hashdu al Sha'abi katika kuendeleza hatua zake dhidi ya kundi hilo la kujitolea la wananchi wa Iraq.

Wizara ya Fedha ya Marekani imemuweka katika orodha yake ya vikwazo Abu Fadak al Muhammadawi Naibu wa Falih al Fayyadh baada ya kumuwekea vikwazo pia mkuu huyo wa Harakati ya Hashdu Shaabi. Abu Fadak al Muhammadawi alichaguliwa kuwa Naibu Mkuu wa Harakati ya Hashdu Shaabi  na kamanda wa maidani wa kundi hilo baada ya kuuliwa shahidi Abu Mahdi al Muhandes. Kabla ya hatua yake hii pia, Marekani ilikuwa tayari imewawaweka katika faharasa yake ya vikwazo makamanda wengine kadhaa wa muqawama akiwemo Qais al Khazali. 

Abu Fadak al Muhammadawi, Naibu Mkuu wa Harakati ya al Hashdu al Sha'abi  

Hatua za Marekani hazikomei tu katika kuwawekea vikwazo makamanda wa muqawama wa Iraq bali nchi hiyo imemuua kigaidi pia Abu Mahdi al Muhandes. Wanamuqawama kadhaa wa Iraq wameuliwa shahidi katika mashambulizi ya kijeshi ya Marekani; huku baadhi ya makundi ya muqawama ya nchini humo likiwemo kundi la  Asa’ib Ahl al-Haq (AAH) pia yakijumuishwa katika orodha ya nchi hiyo eti ya taasisi za kigaidi. Hatua kama hizi zinabainisha chuki na uhasama usio na mwisho wa serikali ya Marekani dhidi ya makundi ya muqawama ya Iraq kama yalivyobainisha makundi ya muqawama kwamba, yana adui asiyekwisha katika eneo la Asia Magharibi. 

Shahidi Abu Mahdi al Muhandes  

Kuhusiana na suala hilo, Mahmoud Ar-Rabi'i Msemaji wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya al Swadiqun  ya Iraq ameandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba: Abu Fadak na makamanda wengine wa Harakati ya Hashdu Shaabi wameitatiza serikali ya Marekani,  kudhalilisha uwezo wake na kupuuza mamluki wake wote. " Harakati ya Kataeb Hizbullah ya Iraq pia imetoa taarifa na kuvitaja vikwazo vya Marekani dhidi ya viongozi wa Hashdu Shaabi kuwa ni ishara ya kuchanganyikiwa Marekani mkabala na kushindwa kwake na muqawama. 

Sababu nyingine inayoipelekea Marekani kuifanyia uhasama Harakati ya Hashdu Shaabi ni kwamba, Washington inataka kuona Iraq ikiwa na jeshi dhaifu na linalolegalega. Kimsingi Marekani haipendelei kuona nchi za eneo na khususan nchi wanachama wa mhimili wa muqawama zikiwa  na majeshi imara na yenye nguvu. Utendaji wa al Hashdu Shaabi na kujumuuishwa kwake rasmi katika muundo wa Iraq kunadhihirisha kuwa, harakati hiyo na makamanda wake wanaweza kuifanya Iraq kuwa na jeshi na vikosi vya ulinzi vyenye nguvu.  

Sababu nyingine kubwa ya chuki ya Marekani kwa kundi la Hashdu Shaabi ni hii kuwa, kwa mtazamo wa Washington; Marekani sasa inashuhudia mchakato wa kuimarika nafasi ya muqawama huko Iraq kwa kuzingatia utendaji uliodhihirishwa na harakati hiyo katika muundo wa madaraka wa Iraq na pia kwa kuzingatia uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa kundi hilo. Katika upande mwingine, Marekani ina fikra hii potofu kwamba kundi hilo linaundwa na wanachama wengi wa Kishia. Washington inadhani kuwa, inaweza kuleta mlingano baina ya makundi ya kisiasa ndani ya Iraq kwa kuidhoofisha Harakati ya Hashdu Shaabi. Ina dhana hiyo potovu licha ya ukweli kwamba wanachama wa Hashdu Shaabi si Waislamu wa Kishia pekee; na kimsingi mwamko wa mapambano ya wananchi hayana muwelekeo wa kimadhehebu katika muundo wa madaraka huko Iraq.  

Nukta ya mwisho ni kuwa, kosa la Marekani ni kwamba inadhani inaweza kuzuia njia ya harakati ya Hashdu Shaabi kwa kuwabana na kuwawekea vikwazo makamanda na  wanachama wa harakati hiyo. Hii ni katika hali ambayo makamanda wa Hashdu Shaabi wanaamini kuwa kitendo cha majina yao kuorodheshwa katika orodha nyeusi ya Marekani ni fahari kwao, na kinazidisha azma na irada yao ya kuendeleza harakati dhidi ya Marekani. Katika upande mwingine, ni dhahir shahir kuwa harakati ya Hashdu Shaabi ina uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa Iraq; kiasi kwamba hata Mustafa al Khadhimi Waziri Mkuu wa nchi hiyo pia juzi alifika katika makao makuu ya harakati hiyo ikiwa ni katika kudhihirisha radiamali yake kwa hatua zinazotekelezwa na Marekani dhidi ya Hashdu Shaabi. Hatua za Marekani zimepelekea kubainika wazi uungaji mkono wa wananchi wa Iraq kwa Hashdu Shaabi; suala ambalo limeshuhudiwa katika safari ya Falih al Fayyadh katika baadhi ya miji ya Iraq ukiwemo mji wa Kirkuk ambapo amekaribishwa kwa shangwe na wakazi wa miji hiyo. 

Mustafa al Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq  

 

Tags