Jan 17, 2021 06:18 UTC
  • Utawala wa Trump waendelea kutekeleza siasa zilizofeli dhidi ya Iran

Ikiwa zimebaki siku chache tu kabla ya kumalizika rasmi utawala wa Rais Donald Trump nchini Marekani, utawala huo umeamua kuongeza mashinikizo ya juu zaidi na vikwazo dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran.

Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ametangaza kuwa Washington imeongeza mashirika kadhaa ya Iran yanayojishughulisha na masuala ya baharini, anga na anga za mbali na vilevile shirika la ndege la Iran katika orodha ya vikwazo ya Marekani.

Pompeo amedai kupitia taarifa kwamba kuimarishwa silaha za kawaida za Iran ni tishio kwa usalama wa eneo na kimataifa na kusema bila kutoa dalili yoyote kwamba mpango wa nyuklia wa Iran inaotekelezwa kwa malengo ya kiraia ni tishio la kudumu kwa usalama wa kimataifa.

Katika miaka kadhaa iliyopita, na baada ya kujitoa katika mkataba wa kimataifa wa nyuklia mashuhuri kwa jila la JCPOA mnamo Mei 2018, serikali ya Washington imekuwa ikitumia uwezo wake wote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika uwanja huo, imetekeleza vikwazo vingi vikali dhidi ya sekta mbali mbali za kiuchumi za Iran. Kwa hakika serikali hiyo katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita imetumia vikwazo hivyo kujaribu kufikia malengo yake dhidi ya Iran na nchi nyingine huru zinazopinga siasa za ubabe na ubeberu za Marekani zikiwemo Venezuela na Russia.

Mike Pompeo

Kwa kutekeleza mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran baada ya kujitoa katika mapatano ya JCPOA, Marekani imejaribu kuilazimisha Tehran iketi kwenye meza ya mazungumzo ili ikubali matakwa yake lakini bila ya mafanikio yoyote. Tovuti ya habari ya Marekani ya Inside Arabia, bila ya kuashiria ukiukaji wa Marekani wa mapatano ya JCPOA imesema kuwa siasa za mashinikizo ya juu kabisa za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran katika miaka miwili iliyopita, zimeshindwa kabisa na kutokuwa na natija yoyote.

Pamoja na hayo lakini bado serikali hiyo inaendeleza siasa hizo dhidi ya mataifa mengine kwa visingizio mbalimbali vya kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kiusalama na hata haki za binadamu.

Alexander Novak, Waziri wa Nishati wa Russia anasema kuhusu suala hilo kwamba: Dunia nzima imechoshwa na vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi tofauti ambazo Washington hairidhishwi na viongozi wake.

Hii ni katika hali ambayo kuenea duniani kwa virusi vya COVID-19 na kutodhaminiwa mahitaji ya kiafya na kimatibabu kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo kumeibua matatizo mengi katika nchi hizo. Kuhusu Iran pia viongozi wake wamekuwa wakizungumzia mara kwa mara taathira hasi za vikwazo vya Marekani katika juhudi zao za kudhamini dawa na vifaa vya afya na matibabu kwa ajili ya kupambana na corona na kutaka vikwazo hivyo viondolewe mara moja ili wapate kuokoa maisha ya raia wao.

Noam Chomsky

Noam Chomsky msomi na mwanafikra mashuhuri wa Marekani amezungumzia suala hilo na kusisitiza kuwa vikwazo hivyo vya Marekani haviwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile na kuongeza kuwa: Chanzo cha vikwazo ni kujitawala na uamuzi wa serikali ya Iran wa kutofuata siasa za Marekani.

Hivi sasa pia na hata ikiwa zimebaki siku chache tu kabla ya kuondoka kwake White House, Trump ameamua kuiwekea Iran vikwazo vipya. Kwa hatua hiyo, anajaribu kuongeza vikwazo dhidi ya nchi ambazo zimekataa kusalimu amri mbele ya siasa za mabavu za Marekani na wakati huohuo kujaribu kufunika kushindwa kwa siasa zake mkabala na Iran kwa kisingizio cha mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani. Ni wazi kuwa kutekelezwa siasa hizo katika siku za mwisho za utawala wa Trump ni juhudi za mwisho za mzama maji zinazofanywa na rais huyo wa Marekani ambaye anaondoka madarakani kwa fedheha kubwa.

Tags