Jan 17, 2021 07:23 UTC
  • Bolton: Mikono ya Trump imejaa damu

Mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani amesema kuwa mikono ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo imejaa damu ya watu wasio na hatia

Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya CNN kuhusiana na uwezekano wa kutokea ghasia na mashambulio ya silaha katika siku ya kuapishwa Joe Biden, rais mteule wa Marekani, Bolton amesema kuwa hatua zisizofaa za Trump zinaweza kusababisha tukio lolote la ghasia na kwamba hiyo ni moja ya dalili kuwa kiongozi huyo mwenye utata hafai tena kuwa rais wa Marekani.

Akiashiria habari ya kukamatwa mtu mmoja aliyekuwa na nyaraka bandia za utambulisho pamoja na silaha nyingi katika kukaribia siku ya kuapishwa rasmi Joe Biden, Bolton amesema kwamba bila shaka jambo hilo linathibitisha ukweli kwamba Wamarekani wanahitajia usalama sehemu hiyo na katika siku hiyo ya kuapishwa Biden.

John Bolton (kushoto) dhidi ya Trump

Bolton vilevile amesisitiza kuwa mtu huyo anapaswa kuhojiwa na kufafanua ni nani alikuwa akishirikiana nao katika suala hilo ili lipate kuwabainikia wazi Wamarekani. Afisa huyo wa zamani wa serikali ya Trump amesema kuhusu uhusiano wa watu waliokamatwa katika ghasia za hivi karibuni mjini Washngton na magenge ya ubaguzi wa rangi na kuongeza kuwa, ni wazi kuwa kuwepo nchini rais ambaye kwa muda wa miezi miwili baada ya kufanyika uchaguzi mkuu na hata kabla ya kufanyika uchaguzi huo amekuwa akisema uongo wa wazi kuhusu uchaguzi huo na kudai kuwa wizi ulifanyika, kunachochea moja kwa moja magenge ya wabaguzi wa rangi na wazuafujo kujihusisha na vitendo vya machafuko na uharibifu.

Trump anatuhumiwa kuhusika na uhalifu mkubwa wa kuchochea wafausi wake kuvamia jengo la Congress ya Marekani tarehe 6 Januari.

Tags