Jan 18, 2021 08:21 UTC
  • Meya wa Washington DC atahadharisha kujiri mashambulizi katika mji mkuu huo

Meya wa mji mkuu wa Marekani ametahadharisha juu ya kujiri mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Washington DC na katika majimbo mengine ya nchi hiyo.

Kuhusu hali ya usalama katika mji mkuu wa Marekani katika wakati huu wa kukaribia kufanyika sherehe za kuapishwa Rais mpya Joe Biden, Bi Muriel Bowser ameeleza kuwa maeneo ya kandokando ya Kongresi yako salama kutokana na kusambazwa askari usalama wa serikali ya federali pamoja na jeshi hata hivyo maizngira ya utulivu kama hayo hayashuhudiwi katika maeneo mengine ya Washington DC na katika majimbo mengine ya Marekani. 

Katika hali ambayo sherehe za kuuapishwa Joe Biden zimepangwa kufanyika Jumatano Januri 20; miji mbalimbali ya Marekani khususan mji mkuu Washington DC yanashuhudiwa hatua kali za kiusama zikiwa zimeimarishwa ikiwemo kuwekwa vizuizi mbalimbali na kusambazwa maelfu ya askari wa gadi ya taifa. 

Wananchi wa Marekani wana wasiwasi mkubwa wa kujiri wimbi jipya la ghasia na vitendo vya utumiaji mabavu katika kukaribia kuapishwa Biden; sawa kabisa na ghasia na uvamizi ulioshuhudiwa katika jengo la Kongresi ya nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa watu watano waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa Jumatano ya tarehe 6 mwezi huu  baada ya wafuasi wa Trump kulivamia jengo la Kongresi ya Marekani wakati wa kufanyika kikao cha Kongresi kilichoitishwa kwa ajili ya kuidhinisha ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba mwaka jana. 

Polisi ya federali ikipambana na wafuasi wa Trump walioshambulia Kongresi 

 

Tags