Jan 19, 2021 07:13 UTC
  • Waziri wa Ufaransa: Siwezi kuvumilia kuona watoto wadogo wanavaa hijabu

Waziri mshauri wa masuala ya uraia wa Ufaransa ametoa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu kwa kutaka uvaaji wa vazi la stara la Kiislamu la Hijabu nchini humo uwekewe mipaka zaidi.

Marlène Schiappa, ametoa matamshi hayo ya chuki dhidi ya Uislamu na kuongezea kusema kwamba, hawezi kuvumilia kuona watoto wadogo wanavaa Hijabu.

Schiappa amependekeza viongezwe vifungu vingine katika sheria inayopiga marufuku wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kuvaa Hijabu katika maeneo ya umma.

Marlène Schiappa

Kabla ya kauli ya waziri huyo, serikali ya Ufaransa ilikuwa tayari imependekeza rasimu ya mswada wa sheria ya "misimamo ya kufurutu mpaka ya Kiislamu", ambayo kwa mujibu wa rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron tayari imeshapitishwa.

Mwaka uliopita wa 2020, serikali ya Paris iliivunja Klabu ya "Mjumuiko Dhidi ya Uenezaji Chuki Dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa" ambayo ni asasi ya kupambana na ubaguzi wa rangi na ubaguzi dhidi ya Waislamu.

Hatua hiyo ya serikali ya Ufaransa ilikosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Katika mwaka huohuo wa 2020, jarida la Charlie Hebdo la nchini humo lilichapisha tena vikatuni vya kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW.

Katika msimamo ulioambatana na hisia za chuki dhidi ya Uislamu, rais Macron alitetea kitendo hicho cha kishenzi kilichofanywa na jarida hilo.

Matamshi na msimamo huo wa rais wa Ufaransa ulikosolewa na kulaaniwa vikali na Waislamu, viongozi na shakhsia wa jamii za Kiislamu duniani kote.

Baada ya kushuhudia ukosoaji na upinzani mkali katika Ulimwengu wa Kiislamu Macron alilegeza misimamo yake dhidi ya Uislamu.../ 

Tags