Jan 20, 2021 12:22 UTC
  • WHO: Spishi mpya ya kirusi cha corona cha Uingereza kimeenea katika nchi zisizopungua 60

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa, aina mpya ya maambukizi ya corona tayari imeena katika nchi kumi nyingine ikilinganishwa na wiki iliyopita.

Shirika la Afya Duniani leo limeripoti kuwa, spishi mpya ya kirusi cha corona kilichogunduliwa nchini Uingereza ambacho kinaenea kwa kasi tayari kimeshaenea katika nchi zisizopungua 60; yaani nchi 10 zaidi ikilinganishwa na wiki iliyopita. Nchi mbalimbali duniani zinahangaika kuhusu namna ya kudhibiti kasi ya maambukizi ya corona hadi hapo chanjo zitakapopatikana kwa wingi. Hii ni katika hali ambayo takwimu za WHO zinaonyesha kuwa, watu zaidi ya milioni mbili wameaga dunia kwa maradhi ya Covid-19 hadi sasa huku kuenea katika nchi zisizopungua 60 duniani kwa spishi hiyo mpya ya kirusi cha corona ikiibua hofu kubwa. 

Spishi mpya ya kirusi cha corona

Taarifa ya kila wiki ya WHO imeeleza kuwa, spishi mpya ya kirusi cha corona kilichoikumba Afrika Kusini kwa jina la 501Y.V2 ambacho kimetajwa kuwa kinaambukiza zaidi lakini hakionekani kuwa hatari kimeripotiwa kuziathiri nchi na majimbo 23 hadi sasa. 

Aina hiyo ya kirusi kipya cha corona kilichogunduliwa kwa mara ya kwanza huko Uingreza katikati ya Disemba mwaka jana kimetajwa na WHO kuwa kinaambukiza zaidi kati ya asilimia 50 hadi 70 kulinganisha na cha awali.