Jan 21, 2021 11:08 UTC
  • Urais wa Biden waanza katika kivuli cha migogoro

Baada ya kumalizika uchaguzi uliogubikwa na utata mwingi, hatimaye Joe Biden ameapishwa kuwa rais wa 46 wa Marekani

Katika hutuba yake ya kwanza akiwa Rais wa Marekani, Biden amsisistiza juu ya masuala muhimu ambayo ni pamoja na 'demokrasia ya Marekani' na 'umoja wa kitaifa' miongoni mwa Wamarekani. Amesema matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni ni ushindi kwa demokrasia na kuitaka mirengo yote ya kisiasa ya nchi hiyo kuweka kando hitilafu zao.

Pamoja na hayo lakini matukio ya miezi kadhaa iliyopita yanathibitisha wazi kwamba kudhoofika misingi ya demokrasia na mapengo ambayo yamedhihiri kati ya matabaka mbalimbali ya Wamarekani ni makubwa kiasia kwamba hayawezi kuzibwa kwa maneno matupu ya rais mpya wa nchi hiyo. Hata hivyo ni wazi kuwa viongozi wa ngazi za juu wa serikali na wanasiasa mashuhuri wa Marekani, bila shaka ukiachilia Donald Trump rais aliyeondoka madarakani na wanasiasa wengine wa karibu yake, wanapasa kusisitiza juu ya umuhimu wa kulindwa umoja wa kitaifa na kuimarishwa misingi ya demokrasia nchini.

Ukandamizaji wa polisi ya Marekani dhidi ya raia weusi

Pamoja na hayo, hotuba zilizotolewa katika nukta mbili tofauti za mji mkuu wa Marekani Washington, yaani moja katika ikulu ya White House wakati wa kuondoka madarakani Trump, na katika Congress, wakati wa kuingia madarakani Joe Biden, zinathibitisha wazi ni kwa kiwango gani jamii ya Marekani imegawanyika. Trump ameondoka madarakani bila kuhudhuria sherehe za kuapishwa Biden naye Biden katika hotuba ya ufunguzi wa urais wake  hakuashiria hata kwa neno moja nafasi ya Trump katika utawala wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo askari walinda-usalama zaidi ya 25,000 waliwekwa sehemu maalumu kulinda usalama wa sherehe hiyo ya kuapishwa Rais Biden na hivyo kuzidi hata idadi ya wageni waalikwa.

Katika miezi michache iliyopita wasiwasi na shaka kubwa imedhihirishwa kuhusu demokrasia ya Marekani na taasisi zinazoilinda. Mbali na madai ya Trump kwamba udanganyifu mkubwa ulifanyika katika uchaguzi wa rais uliofanyika Novemba 3 na hivyo kutilia shaka uhalali wa uchaguzi huo, nafasi kubwa ya pesa na utajiri katika mwenendo wa uchaguzi wa Marekani ni moja ya mambo yanayodhoofisha pakubwa demokrasia ya nchi hiyo. Mbali na hayo, wengi wanaamini kuwa mfumo wa uchaguzi wa Marekani sio wa kidemokrasia kwa kutilia maanani kwamba ni kundi la watu wachache tu ndilo huwa na uamuazi wa mwisho kuhusu nani awe rais wa nchi, kupitia kura za baraza la Electoral College.

Mbali na hayo, migawanyiko ya kisiasa na kijamii inaendelea kuongezeka siku baada ya siku huko Marekani, mfano wa wazi ukiwa ni mauaji ya kikatili yaliyotekelezwa na polisi mweupe wa nchi hiyo dhidi ya raia mmoja mwenye asili ya Afrika katika msimu wa joto uliopita, ambayo yaliitumbukiza Marekani katika mgogoro mkubwa wa ghasia za kijamii, ubaguzi wa rangi na uporaji mali. Katika miezi na wiki za karibuni, kumetolewa maonyo mengi kuhusu kuongeza makundi ya ubaguzi wa rangi na ugaidi wa ndani nchini Marekani, makundi ambayo yaendelea kuimarisha satwa na ushawishi wao katika jamii na taasisi mbali mbali za nchi hiyo.

Ubaguzi wa rangi umezua mgawanyiko mkubwa katika jamii ya Marekani

Kwa kutilia manani hali hiyo, ni wazi kuwa ahadi ya Biden ya kuimarisha demokrasia na kuleta umoja wa kitaifa ndani ya Marekani ni jambo ambalo halitawezekana au kwa uchache litakuwa gumu kufikiwa.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo Francis Fukuyama, mwanafikra mashuhuri wa Marekani na mwandishi wa vitabu vya 'Mwsiho wa Historia' na 'Utambulisho,' huku akibainisha wasi wasi wake kuhusu matukio ya kisiasa na kijamii ya nchi hiyo akasema katika mazungumzo yake na Seymour Hersh, mwandishi wa habari wa nchi hiyo kwamba: Marekani inapasa kusubiri kushuhudia machafuko zaidi.