Hali mbaya barani Ulaya kufuatia kuenea maambukizi ya corona
Serikali za Ulaya zimeshadidisha hatua na vizuizi vya kukabiliana na maambukizi ya corona kufuatia kuenea pakubwa idadi ya watu wenye maambukizi.
Serikali ya Italia imetangaza kuwa italiweka katika ajenda yake ya kazi suala la kuishtaki Kampuni ya Pfizer ya Marekani kutokana na kutotimiza ahadi yake ya kukabidhi chanjo za corona.
Kampuni ya Pfizer imetangaza kuwa, inapunguza kwa muda wa wiki tatu hadi nne kutuma chanjo za corona huko Ulaya kutokana na mabadiliko na ukabarati unaofanyika.

Waziri wa Afya wa Uingereza pia ametangaza kuwa nchi hiyo imesajili rekodi mpya ya vifo vya watu 182 katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Wakati huo huo Taasisi ya Robert Kotch ya Ujerumani pia imewataka wananchi kujiepusha na kupunguza kadiri inavyowezekana safari zao katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Aina mpya ya spishi ya kirusi cha corona au inayofahamika kama kirusi kipya cha corona cha Uingereza tayari inazidi kuenea huko Ujerumani pia. Serikali ya Ufaransa imetoa wito ikitaka kuchukuliwa hatua za kusimamia safari za kuingia na kutoka katika mipaka ya nchi hiyo ili kuzuia maambukizi ya corona.
Wakuu wa nchi za Ulaya leo Alhamisi wamekutana katika kikao chao kwa njia ya video ambapo wamejadili mgogoro wa corona na khususan kuenea maambukizi ya kirusi kipya cha Uingereza. Benki ya Uwekezaji ya Ulaya pia imetahadharisha kupungua pakubwa uwekezaji barani humo kutokana na kuongezeka maambukizi ya corona.