Jan 22, 2021 10:25 UTC
  • Kukataa kuomba radhi Macron kwa jinai ilizofanya Ufaransa enzi za ukoloni nchini Algeria

Ufaransa, ambayo ilikuwa moja ya madola ya kikoloni, ina faili chafu na la kuaibisha kuhusiana na uvamizi, ukaliaji ardhi kwa mabavu na vitendo vya jinai ilivyofanya mnamo karne ya 20 katika nchi ilizozikoloni hususan Algeria.

Algeria ilikoloniwa na Ufaransa kwa muda wa miaka 132; na licha ya miito iliyotolewa mara kwa mara na nchi hiyo kuitaka serikali ya Ufaransa iombe radhi kwa kuikoloni na kwa jinai ilizoitendea nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, lakini rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekataa kufanya hivyo.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Siku ya Jumatano, ofisi ya rais huyo wa Ufaransa ilieleza katika taarifa kwamba, Macron hataomba radhi katu kwa sababu ya Algeria kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu au kwa sababu ya vita vya miaka minane vya umwagaji mkubwa wa damu, ambavyo vilihitimisha enzi za Ufaransa kuikoloni Algeria katika karne ya 20; lakini badala yake atashiriki kwenye hafla tu ya kiuashiriaji kwa madhumuni ya kinachoitwa "kustawisha maelewano na amani" baina ya nchi mbili.

Mnamo miaka miwili nyuma na kupitia taarifa maalumu aliyotoa wakati huo, Emmanuel Macron alikubali rasmi kwamba askari wa Ufaransa walitumia mfumo maalumu ulioratibiwa wa utesaji wakati wa vita vya Algeria; lakini katu hakuomba radhi.

Mateso waliyokuwa wakifanyiwa Waalgeria na wakoloni wa Kifaransa

Baada ya kupita zaidi ya miongo sita tangu vilipomalizika vita vya miaka minane kati ya jeshi vamizi la Ufaransa na wanamapambano wapigania ukombozi wa Algeria, uhusiano baina ya nchi hizo mbili bado haujatengemaa kutokana na jinai zilizofanywa na Wafaransa wakati huo. Ni kutokana na umuhimu wa suala hilo ndipo mwezi Julai 2020, Macron alimwamuru Benjamin Stora, mtaalamu wa historia wa Ufaransa aandae ripoti ya utafiti kuhusu nafasi ya Ufaransa wakati wa enzi za ukoloni na kipindi cha vita vya kupigania uhuru wa Algeria vya baina ya mwaka 1954 hadi 1962. Siku ya Jumatano, ofisi ya rais wa Ufaransa ilitoa taarifa tuliyoiashiria, baada ya rais wa nchi hiyo kupokea ripoti ya utafiti iliyotayarishwa na mwanahistoria huyo.

Profesa Benjamin Stora (kushoto) akimkabidhi rais wa Ufaransa ripoti ya utafiti wake

Ripoti hiyo ya Profesa Stora haijaifanya Paris iombe radhi, isipokuwa imeweza kuweka wazi tu sehemu ya historia chafu ya ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria na kutoa mapendekezo kadhaa kwa ajili ya kuboresha anga inayotawala katika uhusiano wa nchi mbili. Wanahistoria wengi wa Ufaransa na wa nchi zingine za Ulaya wameonyesha kwa ushahidi na nyaraka za kuaminika na kuthibitisha mara kadhaa kwa uchunguzi na utafiti waliofanya, jinsi serikali za Ufaransa za wakati huo zilivyohusika moja kwa moja katika ukandamizaji, mauaji, ubaidishaji na ubaguzi uliofanywa nchini Algeria katika enzi za ukoloni na hasa wakati wa vita vya kupigania uhuru wa nchi hiyo. Pamoja na hayo, hadi sasa hakuna rais yeyote wa Ufaransa aliyekuwa tayari kuiomba radhi rasmi Algeria.

Suala muhimu na la kuzingatiwa hapa ni kwamba, wakati Emmanuel Macron alipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi wa rais wa Ufaransa wa mwaka 2017, na kwa ajili ya kuvutia kura za wafuasi wa mrengo wa kushoto na matabaka ya vijana wa jamii ya nchi hiyo, alizungumzia maafa yaliyotokea wakati wa vita vya uhuru wa Algeria na akasema, Ufaransa inapaswa iiombe radhi Algeria.

Hata hivyo baada ya kuingia Ikulu ya Élysée Juni 2017, Macron alitia ulimi wake puani na kubadilisha msimamo wake wa awali. Inavyoonekana, kiongozi huyo aliandamwa na mashinikizo ya mrengo wa kulia wenye misimamo mikali, yaani chama cha National Rally, mrengo wa kulia wa kati, yaani Rally for the Republic na hata baadhi ya mirengo ya chama chake mwenyewe cha  "The Republic On the Move LREM; na kwa sababu hiyo akaamua kubadilisha waziwazi msimamo wake wa awali kwa kudai kwamba kauli aliyotoa ilinukuliwa kimakosa.

Madhila na masaibu yaliyowapata Waalgeria enzi za ukoloni wa Ufaransa

Lakini pamoja na yote hayo, faili la Ufaransa, inayojigamba kuwa mtetezi mkuu wa haki za binadamu miongoni mwa madola ya Magharibi, la jinai ilizofanya katika vita vya Algeria ni chafu mno na limebeba rundo kubwa la jinai kiasi kwamba hakuna chochote kinachoweza kutetea na kuhalalisha unyama uliofanywa na nchi hiyo.

Mfano wa unyama huo ni ule aliouashiria Abdulmajid Shaykhi , mshauri wa masuala ya historia wa Rais wa Algeria ya kwamba, baada ya kufanya mauaji, Wafaransa walikuwa wakiisafirisha mifupa ya Waalgeria wengi waliouliwa nchini humo na kuipeleka mji wa Marseille huko Ufaransa kwa ajili ya kutengenezea sabuni na kusafishia sukari. Katika kipindi cha miaka minane ya vita vya kupigania uhuru wa Algeria, Wafaransa waliua karibu watu 60,000 miongoni mwa wanamapambano wa Harakati ya Ukombozi wa Taifa ya Algeria (FLN) na wengine wasiopungua milioni moja miongoni mwa raia wa kawaida.../

Tags