Jan 22, 2021 11:52 UTC
  • Trump azidi kuandamwa na majanga, sasa BankUnited imemfungia hesabu zake zote

BankUnited ya Florida huko Marekani imekata ushirikiano wake wote na rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump hatua ambayo inaonekana imetokana na magenge yake kuvamia Baraza la Congress Januari 6, 2021.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, siku moja baada ya Donald Trump kutimuliwa katika Ikulu ya Marekani, White House, BankUnited yenye makao yake huko Florida imeamua kukata uhusiano wake wote naye.

Baada ya magenge ya Donald Trump kuvamia Baraza la Congress siku ya Jumatano ya tarehe 6 Januari, 2021 kwa uchochezi wa Trump, mashirika na taasisi nyingi ndani na hata nje ya Marekani zimeamua kukata uhusiano na rais huyo wa zamani wa nchi hiyo. Magenge hayo ya Trump yalilivamia jengo hilo wakati mabaraza mawili, lile la wawakilishi na lile la seneti yalipokuwa na kikao cha pamoja cha kupasisha ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais wa Marekani wa Novemba 3, 2020.

Magenge ya Trump yalipovamia Congress ya Marekani, Januari 6, 2021

 

BankUnited ambayo iko katika mji wa Miami huko Florida imesema kuwa, imefunga hesabu zote za Trump na kuanzia jana Alkhamisi, Januari 21, 2021, haina tena ushirikiano wa aina yoyote na Trump si wa mikopo wala miamala mingine yoyote.

Hata hivyo BankUnited haikusema ni kwa nini imeamua ghafla moja kukata ushirikiano wake wote na rais huyo wa zamani wa Marekani asiyetabirika na mwenye matatizo mengi.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya benki nyingine kadhaa kama ile ya Deutsche Bank ya Ujerumani na benki nyingine tatu kukata ushirikiano wao wote na Donald Trump ikiwa ni kulalamikia kitendo chake cha kuyachochea magenge yake yavamie Baraza la Congress la Marekani, Januari 6, 2021.

Tags