Jan 23, 2021 08:02 UTC
  • Donald Trump kupandishwa kizimbani Februari 8, 2021

Chuck Schumer, kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Sanate la Marekani amesema kuwa, kesi inayomkabili rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump itasikilizwa tarehe 8 mwezi ujao wa Februari katika baraza hilo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, tarehe 13 Januari 2021, wabunge wa Marekani walipasisha kwa kukra 232 za ndio dhidi ya 197 za hapana, muswada wa kushtakiwa Donald Trump.

Baada ya wafuasi wa Trump kuvamia Baraza la Congress tarehe 6 mwezi huu wa Januari na kufanya mauaji pamoja na kuvunjia heshima maeneo mbalimbali nyeti ya Congress ikiwemo ofisi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Nancy Pelosi, wajumbe wa baraza hilo wamepasisha kwa wingi wa kura muswada wa kushtakiwa rais huyo wa zamani wa Marekani kwa kuchochea uvamizi na mauaji.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 244 ya tangu kuundwa nchi iitwayo Marekani, kwa rais wa nchi hiyo kushtakiwa mara mbili bungeni.

Magenge ya kigaidi ya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump yalioua watu watano ndani ya Congress

 

Baada ya kubwagwa kwenye uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020, Donald Trump alikataa matokeo ya uchaguzi na alichochea wafuasi wake kufanya fujo na mauaji. Hata kwenye sherehe za kuapishwa Joe Biden kuwa rais wa 46 wa Marekani zilizofanyika tarehe 20 mwezi huu wa Januari, Trump alisusia kushiriki.

Katika hotuba yake ya mwisho kama rais wa Marekani, aliyoitoa saa chache kabla ya kutimuliwa  katika ikulu ya nchi hiyo White House, Donald Trump aliwaahidi wafuasi wake kuwa atarejea tena katika ikulu hiyo kwa namna moja au nyingine.

Wachunguzi wanasema kuwa, moja ya umuhimu wa kesi hiyo ni kwamba inaweza kumpiga marufuku Trump kurejea White House katika umri wake wote.