Jan 25, 2021 02:29 UTC
  • Wasi wasi wa viongozi wa Ankara kuhusu kuharibika uhusiano wa Uturuki na Umoja wa Ulaya

Licha ya kuongezeka kila siku hitilafu baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya lakini bado viongozi wa Ankara wanafuatilia juhudi za kupewa uanachama katika umoja huo.

Katika uwanja huo, Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameseisitiza kwamba nchi yake na Umoja wa Ulaya zinapasa kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kulinda uhusiano mzuri uliopo baina ya pande mbili.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi habari akiwa na Joseph Borell, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Mevlut Cavusoglu ametangaza kuwepo kwa mikakati ya kuimarisha uhusiano wa Uturuki na umoja huo kupitia mashauriano kuhusu wakimbizi.

Licha ya juhudi nyingi zilizofanywa na viongozi wa Uturuki kwa ajili ya kuboresha uhusiano na Umoja wa Ulaya, uhusiano wa pande mbili hizo umeendelea kukumbwa na misukosuko hasa katika miongo miwili iliyopita. Baadhi ya misukosuko hiyo inatokana na hitilafu za Ankara na Brussels kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya ugomvi wa Uturuki na Ugiriki katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania na siasa za Uturuki kuhusu nchi za Syria, Libya, Cyprus na hata Karabakh.

Mevlut Cavusoglu

Kuwepo hitilafu kati ya pande mbili hizo kunajiri katika hali ambayo suala la Uturuki kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya ni la muda mrefu. Kwa hakika tunapasa kusema kuwa tokea wakati wa kubuniwa Uturuki mnamo mwaka 1923 hadi sasa, suala la kufanywa nchi hiyo kuwa ya Ulaya ni moja ya mambo ambayo yamekuwa yakiwashughulisha sana wanasiasa wa nchi hiyo.

Pamoja na hayo ombi rasmi la nchi hiyo kutaka kujiunga na nchi za Ulaya lilitolewa mwaka 1964 lakini limekuwa likipingwa mara kwa mara na wakuu wa nchi hizo. Mazungumzo mapya kuhusu suala hilo yalianza kufanyika katika muongo wa 1980. Ombi rasmi la Uturuki kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya liliwasilishwa tarehe 14 Aprili 1987.

Uturuki ilikubaliwa rasmi kuwa mgombea wa kujiunga na umoja huo tarehe 12 Disemba 1999 na mazungumzo kuhusu suala hilo yakaanza tarehe 3 Oktoba 2005.

Pamoja na hayo lakini kungali kuna vizingiti muhimu katika njia ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Uaya. Miongoni mwa vizingiti hivyo ni hitilafu za kiardhi na kisiasa baina ya Uturuki na sehemu inayodhibitiwa na Ugiriki katika kisiwa cha Cyprus na vilevile hitilafu za kisiasa na Ugiriki ambazo zote mbili ni wanachama kamili wa Umoja wa Ulaya.

Hitilafu hizo si tu kwamba hazijatatuliwa bali zinaendelea kuongezeka siku baada ya nyingine. Kuhusu hilo, Jean-Claude Juncker, Mkuu wa zamani wa Baraza la Ulaya amesema: Nimewaonya mara nyingi viongozi wa Uturuki na hasa Rais Racep Tayyib Erdogan mweneyewe kuhusu jambo hili, lakini pamoja na hayo tunashuhudia kwamba kila siku nchi hiyo inaendelea kuwa mbali na vigezo vya Ulaya.

Jean-Claude Juncker

Siku zote Umoja wa Ulaya umekuwa ukiitaka Uturuki ikurubishe siasa zake kwa umoja huo. Pamoja na hayo inaonekana kuwa Uturuki inaendelea kuwa mbali na siasa pamoja na viwango vya Umoja  wa Ulaya. Licha ya yote hayo lakini viongozi wa Ankara wanaendelea kufanya juhudi za kujiunga na umoja huo.

Tags