Jan 25, 2021 12:34 UTC
  • Mkuu wa majeshi Uhispania ajiuzulu kwa kudunga chanjo ya corona bila kuwemo kwenye orodha

Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Uhispania Jenerali Miguel Angel Villaroya amejiuzulu wadhifa wake kufuatia sakata la kupatiwa chanjo ya corona wakati hayumo kwenye orodha ya watu wenye kipaumbele cha kupatiwa chanjo hiyo.

Jenerali Villaroya amejiuzulu wadhifa wa mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Uhispania huku joto la kashfa hiyo inayohusisha maafisa wa jeshi na wanasiasa waliopatiwa chanjo ya corona mapema kabla ya zamu zao likizidi kutokota. Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na mamlaka husika, wafanyakazi wa sekta ya afya na wazee wanaoishi kwenye vituo vya wastaafu ndio wanaopasa kupewa kipaumbele cha kwanza cha kudungwa chanjo ya kinga ya ugonjwa wa Covid-19.

Duru za habari zimeripoti kuwa Waziri wa Ulinzi wa Uhispania Margarita Robles amekubali barua ya kujiuzulu mkuu huyo wa majeshi mwenye umri wa miaka 63.

Jenerali Miguel Angel Villaroya amejiuzulu siku moja baada ya wizara ya mambo ya ndani ya Uhispania kumwachisha kazi luteni kanali mmoja wa jeshi aliyekuwa akihudumu katika gadi ya ulinzi wa kiraia baada ya taarifa za ndani ya wizara hiyo kubaini kuwa naye pia alidungwa chanjo ya corona akiwa hayumo kwenye kipaumbele cha kupatiwa chanjo hiyo.

Waziri wa Ulinzi wa Uhispania ameonya kuwa maafisa wengine kadhaa katika wizara hiyo wanaweza nao pia wakalazimika kujiuzulu baada ya ripoti iliyotolewa kuwatuhumu kuwa walipigwa chanjo ya corona kabla ya zamu zao.

Maafisa kadhaa wa kisiasa waliokumbwa na kashfa hiyo nao pia wamejiuzulu akiwemo Manuel Villegas, mshauri wa afya wa eneo la Murcia kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Uhispania ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa vibaya zaidi na janga la dunia nzima la virusi vya corona, ambapo hadi sasa watu 55,441 miongoni mwa watu milioni mbili na nusu walioambukizwa virusi hivyo wameshafariki dunia.../   

Tags