Jan 31, 2021 07:29 UTC
  • Kujiuzulu mawakili wa Trump kabla hajasailiwa bungeni

Mawakili kadhaa wa timu inayomtetea Donald Trump, Rais wa zamani wa Marekani wamejiuzulu kutoka timu hiyo ikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kusailiwa rais huyo wa zamani katika bunge la Seneti.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, mawakili watano mashuhuri wamejiuzulu kutoka timu hiyo maalumu iliyopangwa kumtetea Trump kwenye bunge la Seneti.

Kanali ya televisheni ya CNN pia imesema kuwa Josh Howard, wakili kutoka jimbo la Carolina Kaskazini, Johnny Gosser na Greg Harris wametangaza rasmi kujiuzulu na kutoshirikiana tena na timu ya mawakili wa Trump katika kumtetea mbele ya Seneti.

Jana asubuhi pia Jarida la Politico liliandika kuwa Butch Bower na Deborah Barbier, mawakili kutoka jimbo la Carolina Kusini walikuwa wamejiuzulu nyadhifa zao katika timu hiyo ya mawakili wanaomtetea Trump.

Wafuasi wa Trump wakivamia jengo la Congress

Rais huyo wa zamani wa Marekani anakabiliwa na tuhuma nzito za kuwachochea wafuasi wake washambulie jengo la Congress ya Marekani mnamo Jumatano tarehe 6 Januari mwaka huu. Tayari wabunge wa chama cha Democrat wameanzisha mchakato wa kusailiwa kwake katika bunge la Seneti.

Iwapo hilo litatimia, hiyo itakuwa ni mara ya pili kwa rais wa Marekani kuwahi kusailiwa mara mbili katika kipindi cha utawala wake wa miaka minne, jambo ambalo halijawahi kutokea tena katika historia ya nchi hiyo.

Tags