Feb 05, 2021 08:02 UTC
  • Uturuki: Marekani ndiyo iliyopanga jaribio lililofeli la mapinduzi ya kijeshi 2016

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki ameituhumu Marekani kuwa ndio iliyopanga jaribio lililofeli la mapinduzi ya kijeshi la mwaka 2016, ambalo serikali ya Ankara imemhusisha nalo khatibu wa Kiislamu Fethullah Gulen anayeishi nchini Marekani.

Suleyman Soylu ametoa tuhuma hizo katika mahojiano na gazeti la Hurriyet linalochapishwa nchini Uturuki na kusisitiza kuwa, Marekani ndiyo iliyopanga jaribio hilo la mapinduzi, Gulen ndiye aliyehusika katika utekelezaji na Ulaya ilifurahia na kuliunga mkono.

"Ni dhahir shahir kwamba Marekani ndio iliyopanga jaribio la Julai 15 na Gulen ndiye aliyetekeleza kwa kufuata maagizo yao", amesisitiza Soylu.

Hata hivyo wizara ya mambo ya nje ya Marekani imekanusha vikali tuhuma hizo na kusema kuwa "hazina ukweli wowote".

Zaidi ya watu 250 waliuawa katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi la Julai 15, 2016 la kumuondoa madarakani Rais Recep Tayyip Erdoğan pamoja na serikali yake, wakati askari waasi walipotumia ndege za kivita, helikopta na vifaru ili kuzishikilia taasisi za serikali.

Fethullah Gulen

Serikali ya Ankara imeitaka mara kadhaa Washington imkabidhi Fethullah Gulen, muitifaki wa zamani wa Erdoğan, ambaye hivi sasa anaishi Pennsylvania, Marekani lakini Washington imekata katakata kumrejesha mpinzani huyo nchini Uturuki ikisisitiza kuwa haijapatiwa ushahidi wa kuaminika wa kumtia hatiani.

Tangu lilipotokea jaribio la mapinduzi ya kijeshi la Julai 2016, serikali ya Uturuki imeshawatia nguvuni watu wapatao 292,000 kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na Gulen na kuwasimamisha au kuwaachisha kazi watumishi wa umma zaidi ya 150,000. Aidha mamia ya vyombo vya habari vimepigwa marufuku na makumi ya wabunge wa upinzani wamefungwa jela kwa kuhusishwa na jaribio hilo.../

Tags