Feb 10, 2021 13:13 UTC
  • Qalibaf: Iran na Russia zinatafakari kuhusu ushirikiano wa miaka 20 na 50 ijayo

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amesema Iran na Russia zinatafakari kuhusu ushirikiano wa kipindi cha miaka 20 na 50 ijayo.

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran ameyasema hayo katika mahojiano na Kanali ya Televisheni ya Rossiya 24 ambapo ameashiria ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Rais wa Russia na umuhimu wa ujumbe huo kwa kusema: "Mabadiliko katika utawala wa Marekani, hayawezi kubadilisha uhusiano wa Tehran na Moscow."

Juzi Spika wa Bunge la Iran aliwasili Moscow kwa lengo la kumkabidhi Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo ujumbe kutoka kwa Kiongozi Muahdamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Qalibaf amesema katika kipindi hiki muhimu cha mfumo wa kimataifa, ushirikiano wa Iran na Russia katika ngazi za kistratijia ni jambo litakaloinua hadhi ya nchi hizi mbili. Ameongeza kuwa ushirikiano wa kistratijia wa Iran na Russia ulianza kufuatia matukuo yaliyoibuka  Syria. Amesema ushirikiano huo ambao ulipelekea kutimuliwa magaidi katika eneo unaweza sasa kupanuliwa katika nyanja zingine.

 Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf (kushoto) akimkabidhi Spika wa Bunge la Russia Duma Vyacheslav Volodin ujumbe maalumu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo

Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa, serikali ya Marekani ambayo haijatekeleza ahadi zake za JCPOA kwa miaka kadhaa haina haki ya kuiainishia Iran masharti. Amesema Marekani inapaswa kwanza kutekeleza ahadi zake kabla ya kuweka masharti na Iran nayo inapaswa kuthibitisha kivitendo kuwa vikwazo vimeondolewa ili hatua kwa hatua ianze kutekeleza ahadi zake katika mapatano hayo ya nyuklia.

Tags