Feb 11, 2021 12:34 UTC
  • Ripoti: Sera mbovu za Trump ziliua maelfu ya Wamarekani

Sera mbovu na ghalati za utawala uliopita wa Donald Trump nchini Marekani zilipelekea mamia ya maelfu ya Wamarekani kupoteza maisha.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya jarida la masuala ya afya la The Lancet linalochapishwa nchini Uingereza. Ripoti hiyo imesema utawala wa Trump ulikumbatia kwa makusudi sera za ubaguzi na za kuligawa taifa hilo kimatabaka, jambo ambalo lilisababisha malaki ya watu kuaga dunia.

Utafiti uliofanywa na wanasayansi 33 na ripoti yao kuchapishwa na jarida la The Lancet umeonyesha kuwa, sera mbovu za utawala wa Trump kuhusu mazingira, mabadiliko ya tabianchi na usalama kazini zilipelekea kunakiliwa vifo 20,000 'vya ziada' mwaka 2019 pekee.

Wanasayansi hao wamesema asilimia 40 ya vifo vya ugonjwa wa Covid-19 vilivyoripotiwa mwaka jana 2020 nchini humo vingeweza kuepukika iwapo utawala wa Trump ungeliweka mikakati madhubuti kama zilivyoweka nchi nyingine za Kundi la G7.

Marekani licha kuwa taifa lililostawi, lakini inaongoza kwa idadi ya vifo na maabukizi ya corona duniani

Wamesema mapuuza ya Trump kwa janga la corona na kuwashajiisha watu kutovaa barakoa kulichangia pakubwa kwa ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

Ripoti hiyo imekosoa ubaguzi katika utoaji wa huduma za afya na hususan kunyimwa au kutopewa huduma nzuri Wamarekani wenye asili ya Afrika waliokumbwa na corona katika utawala wa Trump. 

Tags