Feb 12, 2021 11:45 UTC
  • Sergey Lavrov
    Sergey Lavrov

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amesema kuwa nchi hiyo iko tayari kukata uhusiano wake na Umoja wa Ulaya iwapo itawekewa vikwazo zaidi vinavyotishia uchumi wake kutokana na mizozo inayoendelea baina ya pande hizo mbili baada ya kufungwa jela mpinzani wa serikali ya Moscow, Alexei Navalny na ukandamiza wa maandamano yaliyoanzishwa na waungaji mkono wake.

Sergey Lavrov amesema kuna uwezekano wa kukata uhusiano na Umoja wa Ulaya iwapo Brussels itaendelea kushinikiza vikwazo vikali dhidi ya Moscow. "Tuko tayari kukata uhusiano wetu na EU japokuwa hatutaki kujitenga na jamii ya kimataifa, lakini ukitaka kuwa na amani lazima ujitayarishe kwa ajili ya vita", amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia. 

Matanshi hayo ya Lavrov yametolewa huku ripoti zikisema Umoja wa Ulaya unajadili suala la kuyawekea vikwazo makampuni makubwa ya nishati ya Russia, suala ambalo litakuwa na taathira kubwa kwa uchumi wa nchi hiyo. 

Hivi karibuni Mkuu wa Siasa za Nje wa Ulaya, Josep Borrell alizungumzia suala la kuiwekea vikwazo Moscow akiituhumu serikali ya Rais Vladimir Putin kuwa haina huruma, ni ya kidikteta na inayoogopa demokrasia. Aliyasema hayo baada ya ziara yake mjini Moscow ambako alishindwa kukutana na Alexei Navalny anayeshikiwa jela. 

Josep Borrell

Matamshi hayo ya Borrell yametajwa kuwa ndiyo makali zaidi ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Moscow tangu Russia ilipolitwaa eneo la Cremia mwaka 2014.

Tags