Feb 13, 2021 08:44 UTC
  • Biden atoa ahadi ya kufunga Guantanamo waliyoshindwa kutekeleza na Obama

Rais Joe Biden wa Marekani ameahidi kuwa serikali yake itahakikisha kuwa gereza la kutisha la Guantanamo linafungwa kufikia mwishoni mwa uongozi wake.

Jen Psaki, Msemaji wa Ikulu ya White House amesema Rais Biden ameazimia kulifunga gereza hilo la kijeshi linaloshikilia makumi ya washukiwa wa ugaidi kabla ya kuhitimisha hatamu za uongozi wake.

Hii ni katika hali ambayo, ahadi aliyokuwa ameitoa Barack Obama, rais wa Marekani aliyetangulia, ya kuifunga jela hiyo ya kuogofya iliyoko katika Ghuba ya Guantanamo nchini Cuba mwaka mmoja baada ya kuingia Ikulu ya White House haikutimizwa hadi anaondoka madarakani.

Katika kipindi chote cha miaka minane ya urais wa Obama huku Biden akiwa makamu wake, wabunge wa chama cha Republican walitumia njia mbalimbali kuzuia kufungwa jela hiyo, ikiwemo kukataa kutengwa bajeti kwa ajili ya kushughulikia ufungaji wake au kupinga kuhamishiwa wafungwa wa jela hiyo kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Marekani.

Gereza la Guantanamo

Kwa muda wote wa karibu miaka 18 tangu Gereza la Guantanamo lianze shughuli zake, jumuiya tofauti za kimataifa na makundi mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakitamka bayana kuwa yanayofanywa ndani ya jela hiyo yanakinzana dhahiri shahiri na misingi ya haki za binadamu na haki za msingi za watu wanaoshikiliwa humo.

Jela hiyo imewanyima washukiwa haki ya kubainishiwa makosa na mashtaka yanayowakabili, haki ya kupatiwa mahakama stahiki za kusikiliza kesi zao na haki ya kulalamikia mazingira ya kutisha na yasiyovumilika ya ndani ya jela hiyo.

Tags