Feb 14, 2021 07:50 UTC
  • Pelosi: Warepublican waliomuondoa Trump hatiani ni waoga

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani amewakosoa vikali Maseneta wa chama cha Republican waliopiga kura kumuondoa hatiani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Donald Trump.

Nancy Pelosi amesema, "tulichokiona leo (jana Jumamosi) katika Baraza la Seneti ni kundi la Warepublican waoga ambao hawakuwa na chaguo jingine na walikuwa wanalinda kazi zao."

Faili hilo la kumshtaki Trump katika kikao cha jana liliangushwa kwa kura 57 za Hapana huku Maseneta 43 wakiwemo sita wa chama cha Trump cha Republican wakipiga kura ya kuliunga mkono.

Pelosi amekariri kuwa, waungaji mkono wa Trump ambao mwezi Januari mwaka huu walishambulia jengo la Kongresi ni magaidi wa ndani ya nchi.

Licha ya kuondolewa hatiani, lakini Trump amekuwa rais wa kwanza wa Marekani kusailiwa mara mbili wakati akiwako madarakani. Tarehe 13 Januari, Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipitisha mpango wa kumsaili na kumshtaki Trump kabla ya yeye kuondoka madarakani.

Donald Trump

Baada ya kutolewa hatiani na Seneti, Trump kwa kiburi amejipiga kifua na kusema huu ndio mwanzo wa kuchanua harakati zake.

Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipitisha mpango wa kumsaili na kumshtaki Trump baada ya wafuasi wake kuvamia jengo la bunge la nchi hiyo la Kongresi. Wakati wa hujuma hiyo ya wafuasi wa Trump, Kongresi ya Marekani ilikuwa ikihesabu kura za majimbo ya nchi hiyo na kupasisha ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais.

Hata hivyo Donald Trump ambaye hakuwa tayari kukubali kushindwa, aliwachochea wafuasi wake kushambulia Bunge la Marekani. Watu wasiopungua sita akiwemo afisa wa polisi waliuawa katika hujuma hiyo na wengine kadhaa walijeruhiwa. 

Tags