Feb 16, 2021 02:39 UTC
  • Hofu ya kushadidi matatizo ya kiuchumi na kijamii nchini Marekani

Katika miaka ya hivi karibuni, hali ya kiafya na tiba nchini Marekani daima imekuwa ikizorota na kuvurugika zaidi.

Kusambaa virusi vya Corona katika kipindi cha utawala wa Donald Trump kuliibua changamoto zaidi katika uwanja huo na hivi sasa kunazungumziwa suala la uwezekano wa kutokea janga la kitiba katika nchi hiyo. Bernie Sanders, seneta wa kujitegemea wa jimbo la Vermont ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kukosoa vikali ukosefu wa usawa na uadilifu nchini Marekani na kutangaza kuwa, kwa mujibu wa takwimu Wamarekani milioni 140 wanahesabiwa kuwa wenye kipato cha chini na wengine milioni 92 hawawezi kulipia gharama za huduma za tiba.

Aidha Wamarekani milioni 50 hawana uwezo wa kujidhaminia mahitaji yao ya chakula huku wengine milioni 40 wakiwa katika hatari ya kubakia bila makazi. Hii ni katika hali ambayo, mabilionea 650 wa Kimarekani wamekuwa matajiri zaidi kwa dola trilioni moja katika kipindi cha kuenea virusi vya Corona.

Bernie Sanders, seneta wa kujitegemea wa jimbo la Vermont

 

Seneta Bernie Sanders amekosoa mara chungu nzima hali ya kisiasa na kiuchumi ya Marekani na anaamini kuwa, licha ya kuwa, nchi hiyo kidhahiri ni dola la kidemokrasia, lakini kivitendo ni nchi yenye utawala wa serikali ya wachache (oligarchy) au ule ule utawala unaojulikana kama wa wenye vipawa vya kisiasa, kiuchumi, kijeshi na vyombo vya habari ambao unatanguliza mbele maslahi ya watawala mbele ya maslahi ya umma.

Hali mbaya na ya kusikitisha ya makumi ya mamilioni wa Wamarekani wanaotaabika kwa njaa, kukosa makazi na umasikini na kubwa kuliko yote kutokuwa na uwezo wa kujidhaminia gharama za huduma za matibabu ni ishara ya wazi ya kukabiliwa na matatizo ya kimsingi nchi hiyo inayopigiwa upatu kuwa imepiga hatua kubwa zaidi ulimwenguni. Dhihirisho la hali hii mbaya na ya kimaafa ilitokana na utendaji mbovu wa serikali iliyopita ya Donald Trump na jinsi ilivyoamiliana na mlipuko wa maradhi ya Covid-19.

Marekani ndio taifa lililoathiriwa zaidi na Corona

 

Katika mwaka wa mwisho wa utawala wa serikali ya Trump, virusi vya Corona vilikuwa vimesambaa mno nchini Marekani na hivi sasa nchi hiyo ndio iliyoathiriwa zaidi na janga hilo kuliko taifa jingine lolote lile ulimwenguni. Serikali iliyotangulia haikuweza kabisa kukabiliana na virusi hivyo kutokana na imani potofu za Trump jambo ambalo limeifanya Marekani kuwa nchi nambari moja ulimwenguni iliyoaathiriwa na virusi hivyo.

Wakati wa kuingia na kusambaa virusu vya corona nchini Marekani, Trump alifanya kila awezalo kuonyesha kuwa, hilo ni jambo dogo tu na baadaye akatoa madai ya ajabu na ya kustaajabisha kuhusiana na namna ya kutibu maradhi ya Covid-19. Serikali ya wakati huo ya Trump iliacha kuchukua hatua za dharura na za wakati za kudhibiti na kukabiliana na virusi  vya Corona na hilo kama wanavyoamiani wajuzi wa mambo ndilo lililosababisha Marekani kuwa mhanga mkuu wa maafa ya kibinadamu yanayotokana na Covid-19.

Filihali zaidi ya kesi milioni 28 za maambukizo ya Corona zimesajiliwa nchini Marekani na vifo takribani 500,000, ambapo kwa wastani wa kati watu 4,000 hupoteza maisha kila siku nchini humo kutokana na maradhi ya Covid-19.

Paul Collier, mmoja wa wanauchumi wa Chuo Kikuu cha Oxford anasema: Hali ya mambo nchini Marekani ni mbaya kwa kuzingatia kusambaratika mfumo wa afya na matibabu ambapo kila ambacho kina mafungamano na mfumo wa afya na tiba nchini humo nacho kinakabiliwa na majanga makubwa.

Idadi ya masikini Marekani imeongezeka

 

Ubaguzi katika utoaji wa huduma za afya, kupuuza maagizo ya kitiba na kuchoka wafanyakazi wa sekta ya afya kutokana na wagonjwa wa Covid-19 kuongeza mno, ni sababu kuu zinazotajwa na wajuzi wa mambo kwamba, zinachangia kuendeleza mgogoro wa Corona katika nchi hiyo. Wamarekani wenye asili ya Afrika na wale wenye asili ya Amerika ya Latini wanakabiliwa na hatari zaidi ya vifo vinavyotokana na Corona ikilinganishwa na Wamarekani weupe. Kubaguliwa wagonjwa ambao ni Wamarekani wenye asili ya Afrika, Uhispania au kaumu na jamii za walio wachache ni jambo mbalo linashuhudiwa kwa uwazi kabisa nchini humo.

Wataalamu wa mambo wanatabiri kuwa, Marekani inakabiliwa na msimu mgumu kabisa wa baridi mara hii ambao utaambatana na maambukizo na vifo zaidi vya Corona. Hivi sasa Rais mpya wa nchi hiyo Joe Biden amelipa kipaumbele katika utendaji wa serikali yake suala la kupambana na virusi vya Corona. 

Biden amekiri mara nyingi katika matamashi yake kuhusiana na ukweli huu mchungu unaoikabili Marekani. Kuweko nyufa na tofauti kubwa za kimatabaka zinaoongekeza, kukithiri umasikini unaotokana na kudorora uchumi, ukosefu wa ajira na kuongezeka idadi ya watu wanaobakia bila makazi, matatizo ambayo nayo yanachukua mkondo wa kuongezeka, ni mambo ambayo kwa sasa yanaisumbua mno jamii ya Marekani.

Tags