Feb 23, 2021 02:50 UTC
  • Biden na machaguo yaliyo mbele yake kuhusu Afghanistan

Mullah Baradar, mkuu wa ujumbe wa Taliban katika mazungumzo ya amani ameitaka Marekani iheshimu mapatano iliyofikia na kundi hilo kuhusu kuwaondoa askari wake nchini Afghanistan na akaonya kuwa, Taliban haitavumilia uingiliaji wa majeshi ya kigeni nchini humo.

Mbali na kiongozi huyo, msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid, naye pia ametoa indhari isiyo ya moja kwa moja kwa serikali ya Joe Biden kuhusu uwezekano wa Marekani kukiuka mapatano hayo na akasema: "Ikiwa Marekani itaendelea kuheshimu mapatano, na sisi pia tutaheshimu, vyenginevyo tuko tayari kujitoa mhanga kivyovyote vile kwa ajili ya uhuru wetu."

Kuongezeka maonyo yanayotolewa na viongozi wa kundi la Taliban kunajiri katika hali ambayo, kwa mujibu wa mkataba wa mapatano uliosainiwa baina ya Marekani na kundi hilo, viongozi wa Washington wana muda wa takriban miezi sita kuchukua uamuzi kuhusiana na kuwaondoa  askari wa jeshi la nchi hiyo katika ardhi ya Afghanistan. Muda wa fursa hiyo waliyonayo viongozi wa Marekani umeanza kupungua, kiasi kwamba kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu, endapo Washington itahalifu ahadi iliyowekeana na Taliban itashuhudia hujuma na mashambulio ya kundi hilo dhidi ya askari wa majeshi ya Magharibi. Nazar Mohammad Motmaen, mtaalamu wa masuala ya kundi la Taliban, anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Ikiwa Washington itajitoa kwenye mkataba wake na Taliban, Taliban haitasubiri Marekani irejee kwenye makubaliano, bali itaanzisha tena mashambulio dhidi ya vikosi vya Marekani na NATO."

Joe Biden akihutubia askari wa Marekani

Tab'an sambamba na onyo lililotolewa na viongozi wa kundi la Taliban, mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan amesema, kwa kushauriana na nchi wanachama wa Nato na makamanda wa jeshi la Marekani, Joe Biden anauchunguza mkataba wa makubaliano ya Qatar. Kwa mujibu wa Sullivan, mnamo siku na wiki zijazo, serikali ya Biden itachukua uamuzi kuhusu suala la kuondoka askari wa nchi hiyo huko Afghanistan. Kauli hiyo haijatolewa na Jake Sullivan peke yake, kwani kabla ya hapo, waziri wa ulinzi wa Marekani naye pia alitangaza kuwa Washington itashauriana na waitifaki wake juu ya kuuangalia upya mkataba wa Qatar na kwamba vikosi vya jeshi la nchi hiyo havitafanya pupa ya kuondoka Afghanistan.

Alaa kulli hal sisitizo la mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani na maafisa wengine wa nchi hiyo kuhusu uamuzi atakaochukua Biden kuhusiana na Afghanistan limetolewa katika hali ambayo, kikao cha hivi karibuni cha mawaziri wa ulinzi wa NATO kilimalizika bila kuchukuliwa uamuzi wowote kuhusu kuondoka au kuendelea kuwepo majeshi ya nchi hizo nchini Afghanistan. Hatua ya viongozi wa Marekani ya kutangaza sera mpya za nchi hiyo kuhusu Afghanistan zimeongezeka katika hali ambayo, kulingana na mapatano ya Qatar yaliyofikiwa mwaka uliopita kati ya Washington na Taliban, Washington imeahidi kuwa itahakikisha hadi ifikapo mwezi Mei 2021 askari wote wa kigeni watakuwa wameshaondoka katika ardhi ya Afghanistan lakini kwa sharti la Taliban kutekeleza hatua kadhaa kuhusiana na masuala ya kiusalama.

Mullah Baradar, kiongozi wa mazungumzo wa kundi la Taliban

Hivi sasa muhula ulioainishwa kwa ajili ya kuondoka askari waliosalia wa Marekani nchini Afghanistan unakaribia kumalizika huku washauri wa kijeshi na kiintelijensia wa Washington wakiwa wamemwekea mezani rais wa nchi hiyo Joe Biden machaguo matatu ya kuchagua. Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, chaguo la mwanzo ni pendekezo la kuwaondoa askari wa Marekani kwa mujibu wa muda ulioainishwa, yaani tarehe mosi Mei, hata kama kuondoka huko kutakuwa na maana ya kuanguka serikali ya Afghanistan na kutumbukia nchi hiyo kwenye lindi la vita vya ndani. Chaguo la pili ni kuongezwa muda wa kuwepo askari hao kwa kipindi maalumu, tab'an kupitia mazungumzo na kundi la Taliban; na chaguo la tatu na la mwisho ni kuendelea kubaki nchini Afghanistan kwa muda usiojulikana.

Vyovyote itakavyokuwa, wakati serikali ya Joe Biden inachunguza na kuyapitia upya mapatano iliyofikia na kundi la Taliban, msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Afghanistan Rahamtullah Andar anasema, Marekani haikushauriana na serikali ya nchi hiyo katika kuandaa makubaliano hayo. Andar anasisitiza kuwa, makubaliano hayo hayajasaidia kurejesha amani, kukomesha vita, kuhitimisha umwagaji damu wala kuboresha hali za maisha ya wananchi wa Afghanistan. Anachoashiria msemaji huyo wa Baraza la Usalama wa Taifa la Afghanistan ni mazungumzo ya amani ya Doha, Qatar ambayo hivi sasa yamekwama ukiwa umepita mwezi mzima bila kufanyika kikao au mazungumzo yoyote kati ya wawakilishi wa serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban katika mazungumzo hayo.

Waafghani katika mazungumzo ya amani ya Doha

Kwa ujumla inapasa tuseme kuwa, serikali mpya ya Marekani inayoongozwa na Joe Biden imekusudia kuufikiria upya uamuzi uliochukuliwa na Trump wa kuwaondoa askari wa nchi hiyo walioko Afghanistan. Katika miezi ya karibuni Washington imekuwa ikisisitiza kuwa, kuondoka Afghanistan kutategema hali ya mambo na jinsi Taliban itakavyotekeleza ahadi zake. Inavyoonekana, badala ya makubaliano ya Doha, serikali ya Biden inafikiria kusaini makubaliano ya kistratejia na mkataba wa kiusalama na serikali ya Afghanistan. Na ndiyo maana serikali hiyo mpya ya Marekani inafikiria kutekeleza mpango wa kuondoka hatua kwa hatua sambamba na kulinda maslahi yake nchini humo. Kwa mtazamo wa Joe Biden, China na Russia zingali ni tishio la kistratejia kwa Marekani na kwa sababu hiyo kuwepo kijeshi Washington katika radhi ya Afghanistan ni jambo la lazima.../

Tags