Feb 24, 2021 02:41 UTC
  • Wahanga nusu milioni wa virusi vya corona nchini Marekani, sababu na taathira zake

Baada ya kupita mwaka mmoja sasa tangu kulipotokea mlipukowa ugonjwa wa Covid-19 nchini Marekani na kufeli kwa serikali ya nchi hiyo katika kukabiliana na janga hilo, sasa idadi ya wahanga wa corona imepindukia watu nusu milioni kwa kadiri kwamba, Rais Joe Biden amemuru bendera za nchi hiyo zipepee nusu mlingoti.

Kwa sasa Marekani inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliopatwa na virusi va corona na vilevile idadi kubwa zaidi ya watu walioaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19. Wakati janga hilo la corona lilipoanza, rais wa wakati huo wa Maekani, Donald Trump, alitumia suala hilo kama wenzo wa kisiasa wa kuishambulia China. Trump alivibeza na kivifanyia maskhara na shere virusi hivyo, na hakufanya jitihada za kutosha za kudhibiti maambukizi ya corona. Trump alipinga hata suala la kuweka sheria za kuzuia watu kukusanyika katika maeneo ya umma na karantini za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona na akawafanyia maskhara wataalamu walioshauri watu wavae barakoa. Hali hii sambamba na hali mbaya ya kiuchumi, kushindwa watu wa matabaka mbalimbali hususan jamii za waliowachache kama Wamarekani weusi na Walatino kupata huduma za tiba na dawa, na vilevile uhaba wa zana na vyombo vya tiba, vimeifanya Marekani ivunje rekodi ya kuwa na idadi kubwa zaidi ya waathiriwa na wahanga wa corona duniani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Mzio na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani (NIAID), Anthony Fauci anasema takwimu za watu walioaga dunia nchini Marekani kutokana na virusi vya corona "inastaajabisha". Fauci ameashiria kwamba mgawanyiko wa kisiasa nchini Marekani umechangia sana katika vifo vya zaidi ya Wamarekani nusu milioni na kusema: Maambukizi ya corona yalijitokeza wakati jamii ya Marekani ilipokuwa ikisumbuliwa na mgawanyiko na hitilafu za kisiasa, na uvaaji wa barakoa ulitambuliwa kuwa ujumbe wa kisiasa badala ya kuwa hatua ya kitiba.

Virusi vya corona vinaendelea kuchukua roho za Wamarekani kutokana na hitilafu za kisiasa

Tunaweza kusema kuwa, kwa hakika Donald Trump si tu kwamba hakufuata siasa na sera moja kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, bali pia aliubera ugonjwa huo na kudharau maagizo yaliyotolewa na wataalamu wa masuala ya afya na kuficha hali mbaya ya maambukizi ya Covid-19 na uharibifu wake nchini Marekani. Kwa kadiri kwamba rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden anasema: Idadi ya wahanga na watu waliouawa na virusi vya corona nchini humo imepita ile ya wale waliouawa katika Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.

Japokuwa katika siku za mwishoni mwa utawala wake Trump alijaribu kupunguza walau kidogo hasira za Wamarekani kwa kutangaza habari ya kugunduliwa chanjo ya corona na kutoa ahadi ya kutolewa chanjo hiyo kwa umma kwa ajili ya kudhibiti maambukizi, lakini kivitendo, hadi sasa hakuna uwezekano wa kutolewa chanjo hiyo kwa umma. 

Katika hali ya sasa Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza kuwa kipaumbele cha kanza cha serikali yake ni kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. Hata hivyo inatupasa kusema kuwa, kwa sasa siyo corona pekee inayochukua wahanga na kuua Wamarekani, bali maambukizi ya Covid-19 pia na kutokuwepo mipango mizuri na makini ya kudhibiti ugonjwa huo vimesababisha mpasuko mkubwa wa kitabaka ndani ya jamii ya Marekani ikiwa ni pamoja na kuzidisha umaskini uliotokana na mdororo wa uchumi, ukosefu wa ajira na watu kutokuwa na makazi. Kwa kutia maanani hayo yote wataalamu wa masuala ya tiba wametoa wito wa kutolewa chanjo haraka kwa idadi kubwa zaidi ya Wamarekani kabla ya aina mpya ya virusi vya corona haijasambaa katika maeneo yote ya Marekani na kusababisha maafa ya kutisha zaidi.

Zaidi ya Wamarekani laki tano wameaga dunia kutokana na virusi vya corona

Dakta  Michael Osterholm ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza wa Marekani anasema: Baada ya kushuhudiwa aina mpya ya virusi vya corona katika majimbo mengi ya Marekani inatabiriwa kuwa, wimbi jipya la mambukizi ya aina hiyo litaanza karibuni.

Kwa upande wake, Joe Biden anatarajia kuanza kutekeleza "Mpango wa Uokovu wa Taifa" wenye bajeti ya dola trilioni 1.9 kwa ajili ya kukabiliana na athari mbya zilizosababishwa na maambukizi ya corona. Vilevile ameagiza kutolewa chanjo kwa idadi kubwa zaidi ya wananchi na kuvaa barakoa. Hata hivyo inaonekana kuwa, athari za migawanyiko ya kisiasa na mivutano ya chini kwa chini kati ya asasi za kisiasa za Marekani bado zinaelemea taasisi za kuchukua maamuzi na usimamizi wa masuala ya kukabiliana na maambukizi ya Covid-19.  

Tags