Feb 24, 2021 08:13 UTC
  • Grossi: Iwapo vikwazo vya Iran havitaondolewa, jitihada zote zitaambulia patupu

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amejibu swali kuhusu hatua ya Iran ya kusitisha utekelezwaji Protokali Ziada na kusema, iwapo vikwazo havitaondolewa, basi jitihada zote zitaambulia patupu.

Akizungumza Jumanne, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki amesema: "Iwapo mapatano ya hivi karibuni na Iran hayangefikiwa, basi Iran ingechukua hatua ambazo haingawezekana kuzibatilisha."

Akiashiria safari yake ya hivi karibuni nchini Iran na mapatano yaliyofikiwa baina ya IAEA na Iran, Grossi amesema mapatano hayo yatauwezesha wakala huo  kukagua vituo muhimu vya nyuklia vya Iran. Aidha amesisitiza kuwa IAEA haitaweza kukagua vituo vyote vya nyuklia vya Iran bali itakagua vituo muhimu zaidi. Amesema mapatano mapya ya Iran na IAEA si ya kisheria au kisiasa na wala si mapatano rasmi bali ni maelewano.

Siku ya Jumapili Iran na IAEA zilikubaliana kusitishwa kwa muda utekelezwaji wa Protokali Ziada ambapo IAEA haitakuwa tena na idhini ya kukagua vituo vya nyuklia vya Iran kama ilivyokuwa huko nyuma kwa mujibu wa mapatano ya IAEA. Iran imesema itatekeleza tu majukumu yake ya kawaida kuhusu usalama wa kinyuklia. Hatua hiyo ya Iran imechukuliwa kufuatia sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, kuhusu kukabiliana na vikwazo ambavyo Marekani imeiwekea nchi hii.

Ikumbukwe kuwa, baada ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja na kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei 8 2018, Iran ilijaribu kuyalinda mapatano hayo kwa sharti kuwa upande wa pili nao uyatekeleze. Lakini nchi za Ulaya hazikuchukua hatua zozote za kivitendo za kuyalinda mapatano hayo kama zilivyokuwa zimeahidi.

Kwa kuzingatia hali hiyo, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mnamo Mei 8 2019, kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tokea Marekani ijiondoe katika JCPOA, lilitangaza kuwa, Iran inaanza kupunguza hatua kwa hatua ahadi zake katika JCPOA kwa mujibu wa vipengee 26 na 36 vya mapatano hayo. Hatua hiyo ya Iran ilichukuliwa ili kuwepo mlingano baina ya ahadi na haki zake za kisheria.