Feb 24, 2021 11:38 UTC
  • Borrell akiri kuwa Iran inafungamana na mapatano ya JCPOA na kwamba Ulaya ndio inayoyakiuka

Baada ya kujiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya (Ujerumani, Ufaransa na Uingereza) zimekuwa na utendajikazi hasi katika uga wa kulinda mapatano hayo na pia katika kutekeleza ahadi zao. Hii ni Katika hali ambayo Iran imetekeleza ahadi zake kikamilifu katika mapatano ya JCPOA. Hivi sasa afisa wa ngazi za juu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya amekiri ukweli huo.

Josep Borrell Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya siku ya Jumanne katika kikao cha Baraza la Atlantiki alikiri kuwa, hadi kufikia wakati ambao Marekani ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika JCPOA, Iran ilikuwa inafungamana na mapatano hayo na kwamba hata baada ya hapo iliendelea kufungamana na mapatano hayo. Aidha ameashiria kushindwa kufanya kazi mfumo wa mabadilishano ya kifedha kati ya Iran na Ulaya maarufu kama INSTEX na kukiri kuwa, nchi za Ulaya hazijatekeleza majukumu yao katika mapatano ya JCPOA.

Wakati huo huo, Borell pia ametaka mazungumzo na Iran yazungumzie tu kadhia ya JCPOA. Ameongeza kuwa, JCPOA yalikuwa mapatano ya pande mbili na yanapaswa kurejea katika mkondo wake sahihi. Aidha amesema hivi sasa kipaumbele muhimu zaidi na cha dharura katika ushirikiano wa Ulaya na Marekani ni mapatano ya JCPOA.

Kukiri afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya kuhusu ukweli kuwa Iran imetekeleza ahadi zake katika mapatano ya JCPOA na kwamba Umoja wa Ulaya haujatekeleza ahadi zake katika mapatano hayo ni jambo ambalo kwa mara nyingine linaashiria kuwa Iran imekuwa ikisimamia haki katika katika kadhia ya JCPOA hasa wakati huu.

Baada ya Trump kuiondoa Marekani katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei 2018, nchi za Ulaya hazikuchukua hatua yoyote ya maana ya kuyalinda mapatano hayo. Nchi hizo za Ulaya zilikuwa zikidai mara kadhaa kuwa kwa kuzingatia kwamba mapatano ya JCPOA ni muhimu katika kulinda usalama wa kieneo na kimataifa zilitaka mapatano hayo yaendelee kuwepo na kuahidi kuyalinda.

Hassan Beheshtipur, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Nchi za Ulaya zina hofu kuhusu kusambaratika kikamilifu mapatano ya JCPOA kwani zinaamini kuwa mapatano hayo ni kwa maslahi yao ya kisiasa na kiusalama. Kwa hivyo kulindwa JCPOA ni muhimu kwa nchi za Ulaya."
Pamoja na hayo, kutokana na kuwa nchi hizo zinashinikizwa sana na Marekani na pia kwa kuwa hazina irada ya kutosha, hazijaweza kutekeleza ahadi zao katika JCPOA  hasa katika kutumia mfumo wa mabadilishano ya kifedha na Iran unaojulikana kama INSTEX.

Iran nayo katika kujibu kitendo cha nchi za Ulaya cha kutotekeleza mapatano ya JCPOA, imechukua hatua tano za kupunguza utekelezaji wa majukumu yake katika mapatano hayo. Katika hatua ya hivi karibuni kabisa Iran imesitisha hatua ya kujitolea ya utekezaji wa Protokali Ziada.

Hivi sasa nchi za Ulaya zinapaswa kuchukua hatua za kufidia kuzembea kwao katika utekelezaji wa JCPOA. ili mapatano hayo yaendelee kubakia haki.

Pamoja na hayo, Umoja wa Ulaya  umechukua misimamo ambayo kimsingi inakinzana na muelekeo wa kuhuisha JCPOA.

Katika hali ambayo Borell amesisitiza kuwa mazungumzo na Iran yanapaswa kuzungumzia tu JCPOA, nchi tatu katika Troika ya Ulaya zinataka masuala yaliyo nje ya JCPOA yajumuishwe katika mazungumzo hayo. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametoa matamshi ya kujitakia makuu na kusema uwezo wa Iran wa makombora na sera za Iran katika eneo ni maudhui mbili ambazo zinapaswa kujumuishwa katika mazungumzo yajayo ya JCPOA.

Msimamo huu unaonyesha kuwa, nchi za Umoja wa Ulaya hazina msimamo mmoja kuhusu kadhia ya JCPOA na Iran na hii ni nukta ambayo itatoa pigo kwa nafasi ya umoja huo katika JCPOA na mchakato ujao wa mazungumzo baina ya Iran na 5+1.

Tags