Feb 24, 2021 12:00 UTC
  • Ufaransa yakasirishwa na msimamo wa Pakistan wa kupinga chuki dhidi ya Uislamu

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa imelalamikia matamashi ya hivi karibuni ya Rais wa Pakistan ya kukemea mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa pamoja na kupasishwa sheria inayolenga kukabiliana na Waislamu katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa imemuita balozi mdogo wa Pakistan mjini Paris na kumkabidhi kile ilichokitaja kuwa, kuchukizwa kwake na kitendo cha Rais wa Pakistan cha kulalamikia mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa.

Pakistan ambayo kwa miezi kadhaa sasa haina balozi kamili mjini Paris, mara kadhaa viongozi wake wa ngazi za juu wamejitokeza na kulaani vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa ambavyo vimeshika kasi katika kipindi cha uongozi wa Rais Emmanuel Macron.

Uhusiano wa Pakistan na Ufaransa ulitumbukia nyongo hivi karibuni baada ya matukio ya karibuni huko Ufaransa ya kampeni maalumu za chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo ya bara Ulaya.

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu

 

Hivi karibuni Rais Arif Rehman Alvi wa Pakistan  alikosoa vikali sheria iliyopasishwa hivi karibuni na Bunge la Ufaransa ambayo inabana na kubinya uhuru wa Waislamu.

Sheria hiyo ambayo imepewa jina la “Sheria ya Kuimarisha Thamani za Kijamhuri” inalenga kukabiliana na mambo kadhaa yanayowahusu Waislamu na inaipa serikali haki ya kuingilia mambo ya misikiti na kupeleleleza kamati zinazosimamia misikiti na pia kudhibiti matumizi ya pesa za misikiti na asasi za Waislamu.

Jumuiya ya Waislamu Ufaransa (CFCM) imepinga vikali sheria hiyo na kuitaja kuwa yenye kuwawekea Waislamu vizingiti katika maisha yao yote.