Feb 25, 2021 12:14 UTC
  • Rais Putin: Ugaidi ni tishio hatari zaidi kwa dunia

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema nchi yake itaendeleza vita dhidi ya ugaidi katika maeneo ya mbali kama vile Syria na kuongeza kuwa: "Ugaidi ni tishio hatari zaidi kwa dunia."

Akizungumza katika mkutano na maafisa waandamizi wa Shirika la Usalama la Russia - FSB, Putin amesema ugaidi ni tishio hatari zaidi kwa usalama wa dunia na kuongeza kuwa, kukabiliana na uovu huo kunahitajia hali ya juu ya utajarifu na busara.

Aidha amesema kuwalinda wananchi wa Russia mbele ya vitisho vya ndani na nje ni kipaumbele cha kistratijia nchini humo.

Amepongeza mashirika ya usalama ya nchi hiyo kutokana na mafanikio ya kusambaratisha  njama 72 za majasisi wa kigeni nchini humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Maafisa wa shirika la usalama la FSB la Russia

Putin amesema maadui wa Russia wanatekeleza njama za kuyumbisha maendeleo yake na kusababisha matatizo kwenye mipaka yake, kuchochea kukosekana utulivu ndani ya nchi na kudhoofisha maadili yanayoiunganisha jamii ya Warussia.

Aidha ameongeza kuwa shughuli hizo za madola ya kigeni, ambayo hakuyataja kwa jina, zinalenga kuidhoofisha Russiai na kuiweka chini ya udhibiti wa nje. 

Tags