Feb 26, 2021 02:53 UTC
  • Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan nchini Russia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan ameelekea Moscow, mji mkuu wa Russia kwa madhumuni ya kufanya mazungumzo ya mashauriano na kubadilishana mawazo na viongozi wa Moscow kuhusu mchakato wa amani wa nchi yake na masuala ya kikanda.

Katika safari yake hiyo, Muhammad Hanif Atmar amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa waandamizi kadhaa wa Russia akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov.

Mashauriano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan na viongozi wa Russia kuhusu masuala ya amani ya nchi hiyo yanafanyika katika hali ambayo, kauli iliyotolewa wiki iliyopita na Zamir Kabulov, mjumbe maalumu wa Russia katika masuala ya Afghanistan ya kuunga mkono uundaji wa serikali ya mpito nchini humo imekabiliwa na jibu na radiamali kali ya viongozi wa Kabul.

Hanif Atmar (wa pili kulia) akisalimiana na Sregey Lavrov (wa pili kushoto) baada ya kuwasili mjini Moscow

Kwa mtazamo wa wananchi na serikali ya Afghanistan, mpango wowote ule unaohatarisha nafasi ya serikali ya sasa ambayo imechaguliwa kupitia uchaguzi wa kidemokrasia unakinzana na katiba na haki za wananchi wa Afghanistan.

Mpango wa kuundwa wa serikali ya muda nchini Afghanistan ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na Marekani na baadhi ya nchi zingine kwa lengo la kudhamini matakwa ya kundi la Taliban ili kuhitimisha vita na kufikiwa usitishaji mapigano wa kudumu nchini Afghanistan. Mpango huo umeungwa mkono pia na baadhi ya makundi hasimu ya kisiasa na yanayompinga rais wa nchi hiyo Ashraf Ghani.

Matamshi aliyotoa hivi karibuni mjumbe maalumu wa Russia katika masuala ya Afghanistan ya kuunga mkono uundaji wa serikali ya mpito nchini humo ni kinyume na matarajio waliyokuwa nayo viongozi wa Kabul, ya kuiona Russia ikitoa mchango chanya na athirifu katika mchakato wa amani wa nchi hiyo.

Zamir Kubalov

Katika hali ya sasa, ambapo mazungumzo ya amani na kundi la Taliban yanayofanyika nchini Qatar yameingia kwenye mkwamo, mategemeo ya serikali ya Afghanistan ni kuona nchi za eneo zinaunga mkono misimamo ya msingi ya serikali hiyo.

Takwa la serikali ya Afghanistan kwa jamii ya kimataifa hususan nchi za kanda hii, ni kulishinikiza kundi la Taliban liheshimu makubaliano ya usitishaji vita kwa muda ili kujenga hali ya kuaminiana katika machakato wa mazungumzo baina ya Waafghanistan na kuacha kundi hilo kushurutisha upigaji hatua wa mazungumzo ya kurejesha amani nchini Afghanistan na kutekelezwa mapatano ya Doha yaliyofikiwa baina yake na Marekani.

Wakati serikali ya Afghanistan inataka nchi za eneo zitoe mchango athirifu katika mchakato wa amani wa nchi hiyo kulingana na taratibu zilizoratibiwa na serikali hiyo kuhusu namna ya jamii ya kimataifa inavyopaswa kukabiliana na Taliban katika uga wa mazungumzo ya amani, uungaji mkono ulioonyeshwa na baadhi ya wadau wa eneo ikiwemo serikali ya Russia wa kuunga mkono kuundwa serikali ya mpito nchini Afghanistan si jambo linaloendana na matarajio ya nchi hiyo.

Ni katika mazingira hayo, waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan ameelekea nchini Russia ili katika mazungumzo na baadhi ya viongozi wa nchi hiyo, mbali na kutaja sababu za serikali ya Kabul kupinga mpango wa kuundwa serikali ya mpito, kubainisha pia namna wadau wa eneo na nje ya eneo wanavyopaswa kutoa mchango katika mwenendo wa mazungumzo ya amani ya Afghanistan kulingana na maslahi na usalama wa taifa wa nchi hiyo.

Wawakilishi wa Taliban katika mazungumzo ya amani ya Doha

Viongozi wa Afghanistan wana mategemeo ya kuona nchi mbali mbali zinazotaka kusaidia mchakato wa mazungumzo ya amani ya nchi hiyo zikifanya hivyo kwa kuiunga mkono serikali hiyo halali, katiba ya Afghanistan na msingi wake mkuu wa mfumo wa utawala wa jamhuri; na kuacha kuibua mambo yanayotilia nguvu matakwa yasiyo ya kimantiki ya kundi la Taliban kuhusiana na nafasi ya msingi wa demokrasia.

Matamshi mapya yaliyotolewa na kamanda wa jeshi la nchi kavu la Pakistan kuhusu upinzani wa nchi yake dhidi ya Taliban kuidhibiti Afghanistan kwa namna yoyote ile, ni kilelezo kimojawapo cha matarajio ya serikali ya Kabul  kuhusu namna wadau wa eneo na wa nje wa eneo hili wanavyopaswa kujiingiza katika kadhia ya amani ya nchi hiyo, ambalo ni sisitizo la kujiepusha kushabikia na kuunga mkono matakwa ya kiuchu ya kundi hilo na kuhakikisha uingiaji madarakani wa Taliban unafanyika kupitia kura za wananchi na uchaguzi wa kidemokrasia nchini Afghanistan.../

Tags