Mar 02, 2021 07:44 UTC
  • Mkurugenzi mkuu mpya wa WTO aanza kazi, avunjiwa heshima na gazeti la Uswisi

Mkurugenzi mkuu mpya wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) Bibi Ngozi Okonjo-Iweala aliapishwa rasmi Machi Mosi na hivyo kujaza nafasi hiyo iliyokuwa wazi kwa muda wa nusu mwaka.

Bibi Ngozi Okonjo-Iweala ni Mwafrika wa kwanza kuteuliwa kushika wadhifa huo, na pia ni mkurugenzi mkuu wa kwanza mwanamke.

Wakati huo huo, wanachama wa WTO wamekubaliana kufanya mkutano mkuu ujao wa mawaziri huko Geneva, Uswisi, mwishoni mwa mwaka 2021.

Mkutano huo unaofanyika kila baada ya miaka miwili awali ulikuwa ufanyike Kazakhstan mwaka uliopita, lakini ulicheleweshwa kutokana na janga la virusi vya corona.

Bi. Okonjo-Iweala ana matumaini kwamba mkutano huo utatoa uwanja wa makubaliano kuhusu ruzuku za uvuvi pamoja na mageuzi katika shirika hilo la biashara miongoni mwa masuala mengine.

Huku hayo yakijiri gazeti moja la Uswisi limekosolewa vikali baada ya kuchapisha makala iliyoonekana kumkejeli Bi. Okonjo-Iweala.

Gazeti la Aargauer Zeitung limechapisha makala yenye kichwa cha habari kinachosema ''Bibi huyu mzee atakuwa bosi mpya wa WTO.''

Ngozi Okonjo-Iweala akiwa katika makao makuu ya WTO

Kufuatia ukosoaji mkali, gazeti hilo  limeomba msamaha kwa kuchapisha kichwa hicho cha habari kisichofaa.

Bi. Okonjo-Iweala, mwenye umri wa miaka 66, amekubali ombi la msamaha kutoka gazeti hilo na kusema ni muhimu na muda muafaka kwamba gazeti hilo limeomba radhi.

Aidha amewashukuru viongozi wa kike katika Umoja wa Mataifa pamoja na mabalozi 124 walioko Geneva ambao walisaini taarifa ya kulaani gazeti hilo kwa makala hiyo.