Mar 03, 2021 08:28 UTC
  • Indhari ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu kupungua misaada kwa Yemen

Mnamo Machi 2015, Saudi Arabia, ikishirikiana kwa karibu na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE au Imarati), ilianzisha vita vya kidhalimu dhidi ya watu wa Yemen na hivi sasa wakati vita hivyo vikiingia mwaka wa saba, nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwa mara nyingine kuwa, hali ya kibinadamu Yemen ni mbaya sana na hivyo umoja huo umetoa wito kwa jamii ya kimataifa kutuma misaada ya dharura ili kuzuia kuenea umasikini zaidi na ukata katika nchi hiyo ya Kiarabu.

António Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza Jumatatu katika ufunguzi wa kikao cha kimataifa cha kukusanya misaada ya kifedha kwa ajili ya Yemen, ametoa wito kwa wafadhili kujitolea zaidi ili nchi hiyo ya Kiarabu isitumbukie katika njaa na maafa makubwa.

Amesema: "Leo kukatwa au kupunguzwa misaada ya kibinadamu Yemen ni sawa na hukumu ya kifo kwa wakaazi wa nchi hiyo."

Zaidi ya wawakilishi 100 wa mashirika ya kutoa misaada walishiriki katika kikao hicho ambacho kilifanyika kwa njia ya video ambapo ilitazamiwa kuwa zaidi ya dola bilioni tatu na milioni 84 zingechangishwa kwa ajili ya kutoa misaada ya haraka ya kibinadamu kwa watu wa Yemen.

Kiwango hiki cha msaada unaohitajika ni cha chini zaidi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kimsingi ya watu wanaokumbwa na njaa Yemen. 

António Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Saudi Arabia, kama mwanzishaji wa vita dhidi ya Yemen imeahidi kutoa msaada wa dola milioni 430, UAE dola milioni 230 nayo Marekani ambayo inaziunga mkono nchi hizo mbili katika uvamizi wao dhidi ya Yemen imeahidi kutoa dola milioni 191. Inashangaza kuona kuwa, nchi hizo ambazo ndizo zimepelekea Yemen itumbukie katika maafa makubwa ya kibinadamu sasa zinadai kuwa ziko tayari kuwasaidia Wayemen.

Muungano vamizi wa Saudia unahadaa unaposema unataka kuwasaidia Wayemen kwani hadi sasa ungali umeweka mzingiro wa baharini, ardhini na nchi kavu dhidi ya Yemen na hivyo kuzia kuingia nchini humo bidhaa muhimu na za dharura kama vile vifaa vya tiba na mafuta ya petroli.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa, zaidi ya Wayemen milioni 16 au takribani nusu ya watu wote milioni 29 wa nchi hiyo wanakabiliwa na baa kubwa la njaa.

Aidha takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, watu nusu milioni nchini Yemen wanakaribia kufa kutokana na njaa huku watoto zaidi ya lakini nne walio na umri wa chini ya miaka mitano nao pia wakiwa katika hatari ya kupoteza maisha iwapo hali ya hivi sasa itaendelea.

Hii ni katika hali ambayo baadhi ya nchi za Magharibi kama vile Uingereza ambazo nazo zilikuwa na nafasi muhimu katika kuanzisha na kuendeleza vita vya kidhalimu vya muungano wa Saudia nchini Yemen, na hivyo kupata faida ya mabilioni ya dola kupitia mauzo ya silaha, zimetangaza kupunguza misaada yao kwa Yemen.

James Cleverly, Waziri wa Uingereza nayeshughulikia Masuala ya Mashariki ya Kati akizungumza katika kikao hicho cha Jumatatu amesema nchi yake itatoa msaada wa pauni milioni 87 mwaka huu. Msaada huo umepungua kwa pauni milioni 73 ikilinganishwa na msaada uliotolewa na nchi hiyo katika kikao cha wafadhili wa Yemen mwaka jana.

Wagonjwa wengi Yemen wanakabiliwa na hali mbaya kutokana na ukosefu wa vifaa vya tiba

Kwa maneneo mengine ni kuwa, Uingereza imepunguza kwa zaidi ya nusu misaada yake ambayo imekuwa ikiwatumia watu wa Yemen kupitia Umoja wa Mataifa

Andrew Mitchell mbunge wa Uingereza amesema kupunguzwa misaada kwa Yemen ni jambo linaloibua wasiwasi na kuongeza kuwa: "Uingereza inahusika katika masaibu ya Yemen kwani muungano wa kivita dhidi Yemen unaongozwa na Saudia, hivyo Uingereza haiwezi kukwepa kuhusika na maafa ya kibinadamu nchini humo."

Hatua kama hiyo inamaanisha kuwa Uingereza na nchi za Magharibi kwa ujumla zinapuuza maafa ya kibinaadamu ambayo zenyewe zimeyasababisha kwa kuunga mkono muungano wa kivita wa Saudia dhidi ya Yemen, nchi masikini zaidi katika bara Arabu.

Iwapo kweli nchi za Magharibi zina nia ya kuwasaidia watu wa Yemen, awali zinapaswa kusitisha mara moja uuzaji wa silaha kwa Imarati na Saudia ili nchi hizo mbili chokozi zisiwe na uwezo tena wa kuendelekeza vita visivyo na mlingano dhidi ya Yemen.

Tags