Mar 03, 2021 13:37 UTC
  • UNICEF: Corona imewakosesha fursa ya kupata elimu ya moja kwa moja watoto milioni 168 duniani

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema, janga la dunia nzima la corona liliwakosesha mamilioni ya watoto fursa ya kupata elimu ya moja kwa moja ya kuhudhuria mashuleni katika mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian linalochapishwa Uingereza, UNICEF imetahadharisha kuhusu kiwango kikubwa cha watoto wanaokosa fursa ya kupata elimu na kueleza kwamba, katika mwaka uliopita wa 2020, katika kila watoto saba, mmoja miongoni mwao alikosa kwa zaidi ya asilimia 75 fursa ya kupata elimu kwa njia ya moja kwa moja ya kuhudhuria shule, ukiwa ni wastani wa watoto milioni 214 duniani kote.

Takwimu zilizotolewa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto zinaonyesha kuwa, hali ni mbaya sana katika baadhi ya nchi za Amerika ya Latini na Carribean.

Imeelezwa kuwa, katika nchi hizo, watoto wapatao milioni 98 walikosa fursa ya kupata elimu kwa njia ya moja kwa moja katika mwaka uliopita.

UNICEF imetahadharisha kuhusu taathira hasi za kukosa elimu na mafunzo kwa watoto kutokana na kufungwa skuli katika maeneo mbalimbali duniani.

Kusambaa kwa virusi vya corona na kukosekana chanjo na dawa zenye athari kamili ya kudhibiti kirusi hicho kumezifanya nchi duniani zilazimike kuchukua tahadhari za kiafya ikiwemo kuchunga protokali za maingiliano ya kijamii na kufunga shule na shughuli mbali mbali za ajira za kupatia kipato.

Takwimu zinaonyesha kuwa, hadi sasa zaidi ya watu milioni 115 wameambukizwa virusi vya corona duniani kote.../

Tags