Mar 03, 2021 13:42 UTC
  • Ilhan Omar awasilisha mswada wa vikwazo dhidi ya Bin Salman akisema ni 'kigezo cha kupimia utu wa Marekani'

Mbunge wa Marekani wa jimbo la Minnesota kwa tiketi ya chama cha Democratic amewasilisha mswada wa vikwazo dhidi ya Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia kwa kuhusika kwake katika mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud.

Katika taarifa aliyotoa jana, Ilhan Omar amesema "hiki ni kipimo cha utu wetu" na akafafanua kwa kusema "kama ni kweli Marekani inaunga mkono uhuru wa kutoa maoni, demokrasia na haki za binadamu hakuna sababu yoyote ya kutomwekea vikwazo Mohammad bin Salman, mtu ambaye vyombo vyetu wenyewe vya intelijensia vimebaini kuwa aliidhinisha mauaji ya mkazi wa Marekani na mwandishi wa habari wa Saudia Jamal Khashoggi."

Mswada uliopendekezwa na mwakilishi huyo wa chama wa Democratic katika Baraza la wawakilishi la Marekani unataka kuzuiwa mali za Bin Salman, kuzuiliwa miamala yote ya mabadilishano inayohusiana na Marekani, kuhakikisha mrithi huyo wa ufalme wa Saudia haruhusiwi kuingia Marekani, kuhakikisha hawi na uwezo wa kupata viza na maslahi ya uhamiaji pamoja na kubatilisha viza zozote alizonazo hivi sasa za kuingia nchini humo.

Bin Salman (kulia) na hayati Jamal Khashoggi

Ijumaa iliyopita, Ofisi ya Mkurugenzi wa Intelijensia ya Taifa (ODNI) iliweka hadharani iliyokuwa ripoti ya siri iliyotayarishwa na mashirika ya ujasusi ya Marekani ambayo ilimbebesha lawama Mohammad bin Salman ya kupanga operesheni maalum mwaka 2018 ya mauaji ya Jamal Khashoggi, raia wa Saudi Arabia mkazi wa Marekani aliyeuliwa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki.

Hayo yanajiri huku serikali ya Joe Biden ikisisitiza kuwa itawazuia kuingia Marekani baadhi ya watu 18 waliotajwa katika ripoti ya ODNI, lakini haitaweza wazi majina yao. Ni baidi kwamba jina la Bin Salman, ambaye ndiye hasa anayeongoza Saudia hivi sasa litakuwemo kwenye orodha hiyo.../