Mar 04, 2021 04:16 UTC
  • Newsweek: Marekani yumkini ikawa kituo kikuu cha kueneza fikra za kibaguzi

Jarida la kila wiki la Newsweek la Marekkani limeandika kuwa, waitifaki wa serikali ya Washington wana wasiwasi kwamba yumkini fikra na mitazamo ya mirengo yenye misimamo mikali ya kulia ikasambaa pia katika nchi hizo kutoka Marekani.

Jarida hilo lieandika kuwa, matukio ya karibuni nchini Marekani, likiwemo shambulizi la wafuasi wa Donald Trump dhidi ya majengo ya Kongresi, yamewatia wasiwasi waitifaki wa Marekani juu ya uwezekano wa kupanuka na kuenenea zaidi fikra za kupindukia mipaka za mrengo wa kulia na mitazamo ya makundi ya kibaguzi ya wazungu wanaojiona kuwa bora zaidi na wanadamu wengine.

Jarida la Newsweek limeandika kuwa, viongozi wa nchi za dunia na makundi ya kutetea haki za binadamu waliyatazama matukio ya tarehe 6 Januari nchini Marekani kwa jicho la wasiwasi na hofu, na matukio hayo yamesadikisha tahadhari zilizokuwa zikitolewa hapo awali kwamba, tishio kubwa zaidi la usalama wa taifa wa Marekani liko ndani ya Marekani kwenyewe. 

Jarida hilo limesisitiza kuwa, washirika wa Marekani wameshuhudia wimbi kubwa la fikra za uchupaji mipaka mamboleo na wanaelewa vyema kwamba, matangazo ya vyombo vya habari vya Marekani yanafika maeneo mbalimbali ya dunia; kwa msingi huo kuna wasiwasi kuhusu hatari ya kupelekwa fikra hizo za misimamo mikali katika nchi zao au kuundika mseto wa fikra hizo za kibaguzi na fikra mfano wake za maeneo mengine.

Tarehe 6 mwezi Januari mwaka huu wafuasi wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, walivamia majengo ya Kongresi ya nchi hiyo na kuvuruga kikao cha Kongresi ambacho kiliitishwa kwa lengo la kupasisha ushindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba 3 nchini humo. 

Trump ndiye aliyewachochea wafuasi wake kufanya shambulio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa huko Marekani baada ya kubwagwa katika uchaguzi wa rais.

Watu watano waliuawa katika shambulio hilo na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Tags