Mar 04, 2021 13:16 UTC
  • Marekani kuhusu Israel; punda ni yule yule soji tu ndilo lililobadilika

Kama ilivyo kwa serikali zote za Marekani, serikali ya hivi sasa ya nchi hiyo nayo pia inaukingia kifua kwa kila hali utawala wa Kizayuni wa Israel. Tukio la karibuni kabisa ni kwamba serikali hiyo imepinga kufanyika uchunguzi kuhusu jinai za kivita za utawala wa Kizayuni.

Edward "Ned" Price, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema kuwa amekatishwa tamaa na uamuzi wa Mahakama ya Kiamtaifa ya Jinai ICC wa kufanya uchunguzi kuhusu jinai za kivita za Israel.

Amesema, Wapalestina hawajatimiza masharti ya kuwa taifa lenye nchi yao, hivyo hawana haki ya kuwa wanachama wa Mahakama ya Kiamtaifa ya Jinai ICC wala kushiriki katika mahakama hiyo kama serikali na wala kutoa ushauri na kuwasilisha mashtaka ya aina yoyote ile.

Jana Fatou Bensouda Mwendesha Mashataka Mkuu wa ICC alitoa tamko na kusema kuwa, zoezi la mahakama hiyo la kuchunguza jinai za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel, limeanza.

Rais wa Marekani, Joe Biden

 

Mwendesha Mashtaka Mkuu huyo wa ICC amesema kuwa, uchunguzi huo unafanyika kwa uhuru na haupendelei upande wowote na tena unafanyika bila ya woga.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake The Hague, Uholanzi mwezi uliopita iliwapa ushindi wananchi wa Palestina kwa kupasisha kuwa, mahakama hiyo imetimiza masharti na ina haki ya kufuatilia mashtaka yaliyofunguliwa kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na utawala wa Kizayuni huko Palestina.

Licha ya kuweko upinzani mkubwa hasa kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake, lakini mahakama hiyo ya kimataifa imeamua kulifuatilia suala hilo na sasa hivi imeingia kwenye hatua ya kuchunguza jinai za kivita zilizofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.