Mar 05, 2021 02:29 UTC
  • Kuanza kampeni kubwa ya vikwazo ya serikali ya Biden dhidi ya Russia

Uhusiano wa Marekani na Russia katika serikali mpya ya Marekani na wakati huu wa uongozi wa Joe Biden umezidi kuwa mbaya. Serikali ya Biden mbali na kudhihirisha misimamo iliyodhidi ya Russia, hivi sasa imeanzisha kampeni kubwa ya vikwazo dhidi ya Moscow.

Wizara ya Biashara ya Marekani Jumanne wiki hii iliyaweka mashirika 14 binafsi ya Russia, Ujerumani na Uswisi katika orodha yake ya vikwazo kwa kisingizio cha kustawisha silaha za nyuklia na za kemikali. Hatua hii imechukuliwa baada ya ile ya mwezi Agosti mwaka jana wa 2020 ambapo Marekani iliziweka taasisi tano za serikali ya Russia katika orodha hiyo kwa kisingizio kwamba zinasaidia miradi ya silaha za kemikali na kibiolojia ya Russia. Orodha hiyo itazuia usafirishaji, uuzaji mpya na utumaji wa bidhaa kwa mashirika na taasisi hizo chini ya sheria za Idara ya Kusimamia Uuzaji Bidhaa Nje ya Nchi. 

Wizara ya Fedha ya Marekani Jumanne wiki hii pia ilitoa taarifa ikitangaza kuwa, imewawekea vikwazo maafisa saba wa ngazi ya juu wa serikali ya Russia kwa kuhusika na faili la madai ya kupewa sumu Alexei Navalny, kiongozi wa wapinzani wa serikali ya Russia. Aidha katika hatua nyingine, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imetangaza kuwa, ni marufuku kuiuzia Russia zana za kijesshi kutoka Marekani. Kwa mujibu wa tangazo hilo la Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani, vikwazo hivyo vitaendelea kutekelezwa kwa miezi 12 ijayo. Vikwazo hivyo vya Washington vimetekelezwa kwa wakati mmoja na vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya viongozi mbalimbali wa Russia wakiwemo Mwendesha Mashtaka Mkuu, Mkuu wa Kamati ya Utafiti, Mkuu wa Idara ya Huduma za Shirikisho na Mkurugenzi wa Gadi ya Taifa ya nchi hiyo. 

Alexei Navalyn, mpinzani mkuu wa serikali ya Russia 

Kutangazwa vikwazo hivi vikubwa dhidi ya Moscow kuna maana ya kushadidi vita baridi kati ya Marekani na Russia. Kwa utaratibu huo, kama ambavyo viongozi wa ngazi ya juu wa Russia wanasisitiza kwamba, si tu hakuna matarajio ya kuboreka uhusiano kati ya Moscow na Washington katika kipindi cha utawala wa Biden, bali pia ushahidi unaonyesha kuongezeka sana mivutano na kuharibika zaidi uhusiano kati ya nchi mbili hizo.  

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Dmitry Terenin anasema: Katika muda wa miaka minne iliyopita Russia ilikuwa mlengwa wa siasa za ndani za Marekani. Kwa msingi huo, mpambano huo utaendelea kupamba moto zaidi katika utawala wa Biden. Joe Biden anazidisha hitilafu kati ya Marekani na Russia ambazo zilionekana kuwa baridi na zisizoeleweka wakati wa utawala wa Trump na anatumia masuala kama demokrasia na haki za binadamu dhidi ya Russia.  

Viongozi wa serikali ya Biden, kupitia misimamo na matamshi yao ya mara kkwa mara, wamekuwa wakiitaja Russia kuwa ni adui na kutoa wito wa kukabiliana eti na siasa na hatua za Moscow. Suala hili linaonehaka kushadidi zaidi hususan kwa kutilia maanani madai ya Wademocrat nchini Marekani kwamba Russia iliingliia uchaguzi wa rais nchini humo mwaka 2016 uliopelekea kuingia madarakani serikali ya Trump, na pia  madai hayo kukaririwa zaidi katika uchaguzi wa rais wa mwaka jana. Katika upande mwingine, pamoja na kuwa Moscow imefikia makubaliano na Washington juu ya suala la kurefusha mkataba wa New Start kwa miaka mingine mitano, lakini serikali ya Biden imekuwa na dhana mbaya kuhusu malengo ya kijeshi na sera za silaha ya Russia hususan kuhusiana na silaha za nyuklia, kemikamli na zile za biolojia za nchi hiyo, na katika uwanja huo imeyawekea vikwazo mashirikka ya Kirussia na yale yenye mfungamano na Russia kwa kisingizio cha eti kuizuia Russia isipate teknolojia nyeti ya Marekani. Wizara ya Biashara ya Marekani imedai kuwa, iwapo Russia itapata teknolojia hiyo kuna uwezekano wa kushuhudiwa shughuli haribifu za silaha za kemikali na silaha nyingine za maangamizi ya halaiki.

Mkabala na madai haya, Russia imesisitiza kuwa Marekani haina haki ya kutoa somo kwa nchi nyingine baada ya kujitoa katika mikataba na mapatano mbalimbali ya kimataifa yanayopiga marufuku uenezaji na usambazaji wa silaha za mauaji ya halaiki duniani.

Katika upande mwingine, Marekani siku zote imekuwa ikiingilia masuala ya ndani ya Russia na kuiwekea mashinikizo nchi hiyo kwa kisingizio cha eti kuwaunga mkono wapinzani wa Moscow na kutetea haki za binadamu. Katika uwanja huo, wenzo mpya unaotumiwa sasa na nchi za Magharibi ikiwemo Marekani ili kupanua kampeni ya vikwazo dhidi ya Russia ni suala la kutiwa mbaroni na kuhukumiwa Alexei Navalny, mpinzani wa serikali ya Moscow anayeungwa mkono na nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo, na kwa kuzingatia kuungana tena Ulaya na Marekani, inatazamiwa kuwa nchi hizo zitazidisha hatua na mashinikizo dhidi ya Russia  katika kipindi hiki cha utawala wa Joe Biden. 

Rais Joe Biden wa Marekani  

 

Tags