Mar 05, 2021 02:31 UTC
  • Rais Xi: Marekani ndilo tishio kuu kwa ustawi na usalama wa China

Rais Xi Jinping wa China amesema Marekani ndilo tishio kubwa zaidi kwa maendeleo na usalama wa nchi hiyo ya Asia.

Xi amenukuliwa akisema hayo na gazeti la New York Times na kuongeza kuwa, "chimbuko kuu la vurugu katika dunia ya leo ni Marekani. Marekani ndilo tishio kuu kwa ustawi na usalama wa China."

Rais wa China ameeleza bayana kuwa, nchi za 'Mashariki' zinastawi na kukuwa kwa kasi kubwa, huku zile za 'Magharibi' zikididimia na kuporomoka.

Matamshi ya Rais Xi Jingping wa China yanaonekana kuwa jibu kwa kauli ya Antony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyedai hivi karibuni kuwa, China ndiyo changamoto kuu ya kijiopolitiki katika karne ya 21.

Biden na Xi

Katika mazungumzo yake ya kwanza na Rais Joe Biden wa Marekani, Rais Xi alisema makabiliano baina ya Marekani na China yatakuwa maafa makubwa na kwamba nchi mbili hizo zinapaswa kutafutia ufumbuzi mizozo iliyopo kwa njia za amani.

Biden anaituhumu Beijing kwa ukiukaji wa haki za binadamu na kuwakandamiza waandamanaji wa Hong Kong, madai ambayo serikali ya China imepuuzilia mbali.

 

 

Tags