Mar 05, 2021 03:22 UTC
  • UN: Vikwazo vya upande mmoja vya Marekani ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametangaza kuwa, matangazo ya hali ya dharura ya serikali ya Marekani ambayo yamekuwa kisingizio cha kuweka vikwazo vya upande mmoja dhidi ya nchi mbalimbali yanapelekea kukiukwa haki za binadamu.

Taarifa iliyotolewa na wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa, vikwazo vya Marekani vinavyotangazwa katika hali ya dharura vinakiuka haki nyingi za binadamu katika nchi za China, Cuba, Haiti, Iran, Nicaragua, Russia, Syria, Venezuela, Zimbabwe na katika nchi nyingine za dunia.

 Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa Alena Douhan na mtaalamu wa kujitegemea wa haki za binadamu wa umoja huo Obiora C. Okafor wamesema katika ripoti hiyo kwamba, matangazo ya hali ya dharura ya Marekani mara nyingi yamekuwa yakikiuka na kukanyaga sheria za kimataifa za haki za kiraia na kisiasa.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kuwa, matangazo hayo ya hali ya dharura ya serikali ya Marekani yamekuwa kisingizio cha kutekeleza vikwazo visivyo na mpaka.

Wataalamu hao wa haki za binadamu wa UN wameitaka Marekani iheshimu majukumu yake kwa mujibu wa sheria za kimataifa zinazolinda haki za kiraia na kisiasa na kuzuia athari mbaya za ukiukwaji wa haki za binadamu.  

Mwaka 2018 serikali ya Donald Trump huko Marekani ilijiondoa katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia JCPOA kwa kifupi na kuanza kutekeleza vikwazo vua kidhalimu dhidi ya taifa la Iran.