Mar 05, 2021 07:48 UTC
  • Maria Zakharova
    Maria Zakharova

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russia amesema kuwa nchi yoyote inayoshindana na Marekani katika uwanja wowote ule hutambuliwa na Washington kuwa ni nchi adui.

Maria Zakharova ameyasema hayo baada ya matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, kuhusiana na wapinzani wakuu wa nchi hiyo, na kuongeza kuwa: Wakati wowote nchi fulani inapoipiku na kuiacha nyuma Marekani katika masuala ya kiuchumi, teknolojia na ustawi na maendeleo ya anga kama China, Washington hupiga kengele ya kuitangaza nchi kama hiyo kuwa adui wake.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russia amesema kuwa, Moscow inataka kuwepo ushindani wa kiadilifu na kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kama jambo hilo linavyosadiki kuhusiana na China. 

Jumatano iliyopita Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken aliashiria vipaumbele vya siasa za nje za serikali mpya ya nchi hiyo na kusema serikali ya Joe Biden inaitambua China kuwa ndiyo changamoto kuu ya kijiopolitiki katika karne ya 21. Blinken aliongeza kuwa, Russia, Iran na Korea Kaskazini pia ni miongoni mwa changamoto kuu za Marekani. 

Tags