Mar 05, 2021 07:48 UTC
  • Wasomi 26 wataka kufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusu chanzo cha virusi vya corona

Gazeti la Wall Street Journal la Marekani limetangaza kuwa, wasomi 26 wameandika barua ya wazi wakitaka kufanyike uchunguzi mpya wa kimataifa kuhusu chanzo cha virusi vya corona.

Wito huo umetolewa huku kukiwepo shaka kuhusiana na matokeo ya awali ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa Shirika la Afya Dunia (WHO) kuhusu chanzo cha virusi hivyo.

Gazeti hilo limeandika kuwa, kutokana na shaka iliyopo kuhusu chanzo cha virusi vya corona na malumbano makubwa baina ya Marekani na China kuhusiana na virusi hivyo vilivyodhihiri kwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan huko China mwishoni mwa mwaka 2019, timu ya Shirika la Afya Duniani iliyopewa jukumu la kuchunguza kadhia hiyo imeamua kuchelewesha matokeo ya awali ya uchunguzi wake huko China.

Tarehe 12 Februari Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus alitangaza kuwa timu ya uchunguzi ya shirika hilo iliyotumwa China itatangaza matokeo ya awali ya uchunguzi wake katika kipindi cha wiki moja na kusambaza matokeo kamili wiki kadhaa baadaye. Hata hivyo ripoti ya matokeo hayo haijatolewa hadi hivi sasa.

Tedros Adhanom Ghebreyesus

Kwa msingi huo kundi la wasomi 26 limeandika barua ya wazi likitaka kufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusu chanzo halisi cha virusi vya corona likidai timu ya WHO haikupata taarifa za kutosha za kuiwezesha kuchunguza chanzo halisi cha virusi hivyo.

Awali timu ya WHO iliyotumwa Wuhan ilitangaza kuwa, ni jambo lililo mbali kuwa virusi vya corona viliibuka kutoka kwenye maabara moja ya utafiti katika mji huo.

Zaidi ya watu 116,248,279 wameambukizwa virusi vya corona kote dunia hadi hivi sasa na 2,582,140 miongoni mwao wameaga dunia kutokana na virusi hivyo. Marekani inaongzoa duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa na vilevile idadi kubwa zaidi ya watu walioaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.  

Tags